Polisi yamshikilia DED Igunga, kusafirishwa kwenda Kigoma

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Kabla ya kuhamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Msabila alikuwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Tabora. Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Athumani Francis Msabila anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora akisubiri kusafirishwa kwenda Mkoa wa Kigoma kwa hatua zaidi za kisheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao ameiambia Mwananchi leo Novemba 6, 2023 kuwa mkurugenzi huyo anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Igunga.

‘’Ni kweli tunamshikilia akisubiri kusafirishwa kwenda mkoani Kigoma anakokabiliwa na kesi ya kujibu,” amesema Kamanda Abwao

Ingawa Kamanda Abwao hakuwa tayari kuzungumzia kwa undani suala hilo, Msabila ni kati ya watu 10, wakiwemo watendaji na watumishi wa umma wanaodaiwa kuhusika kwenye mtandao wa kuhamisha fedha za umma kinyume cha sheria alipokuwa mkoani Kigoma.

Kabla ya kuhamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Msabila alikuwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Pamoja na wenzake, Msabila aliyetiwa mbaroni muda mfupi baada ya kurejea Igunga akitokea mjini Dodoma alikoenda kikazi walitajwa kwenye taarifa ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kufuatilia tuhuma za uchepushaji wa fedha katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Kigoma Septemba 20 hadi 22, 2023, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipata taarifa ya tukio la fedha za umma kuingizwa kwenye akaonti ya Amana ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kutoka Tamisemi na kisha kuhamishwa baada ya muda mfupi bila kujulikana zilikopelekwa na zimetumikaje.

Kutokana na taarifa hizo, Waziri Mkuu aliagiza uchunguzi uliobaini uwepo wa mtandao wa watu wanaohusika na uchepushaji wa fedha hizo za umma huku zaidi ya Sh463 milioni zikigundulika kutumwa Halmashauri ya Kigoma Ujiji bila kuwemo kwenye moango wa bajeti ya halmashauri na hazijawahi kuombewa matumizi kama bajeti ya ziada.