Polisi yaua ‘panya road’ sita Dar

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro akiwaonyesha waandishi wa habari  silaha walizowakamata nazo wahalifu maaarufu 'panya road' baada ya kupambana nao katika eneo la Makongo. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kuwa limewaua watu sita wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha maarufu ‘panya road’ eneo la Makongo.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kuwa limewaua watu sita wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha maarufu ‘panya road’ eneo la Makongo.

Pia, Jeshi hilo linawatahadharisha wahalifu wanapotakiwa kujisalimisha wakati wa ukamataji wafanye hivyo. 

Hayo yamesemwa leo Jumapili Septemba 18, 2022 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa watu hao wamefariki dunia wakati wakipelekwa hospitali baada ya kujeruhiwa kwa risasi.

Kamanda Muliro amesema “Jana majira ya saa nne na robo eneo la Makongo area 4 tulipata taarifa kutoka Kaa wananchi wema wakisema wahalifu hao wamepanda Noah wakitokea Mabibo walijipanga kwenda Makongo kufanya uhalifu ilipofika saa nne na robo askari wakakutana na gari hilo na walilisimamisha na wahalifu wale waliamrishwa watoke nje ya gari na wakatoka na mapanga wakitaka kujeruhi askari,

Jeshi la Polisi limesikia vilio vya wananchi na litahalikisha watu hawa hawaendelei, tutayafikia makundi yote kwa haraka na operesheni hii kali itaendelea tunatoa onyo vikundi hivi viko vinne vitano na tutavifikia Kwa haraka” amesema.