Polisi Zanzibar yakamata watu tisa kwa tuhuma za magendo

Polisi Zanzibar yakamata watu tisa kwa tuhuma za magendo

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharib Unguja linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kutaka kusafirisha magendo ya vyakula na bidhaa mbali mbali kwenda Tanzania bara 

Unguja. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharib, Unguja limefanikiwa kuwakamata watu tisa kwa tuhuma za kutaka kusafirisha magendo
Akitoaa taarifa kwa waandishi wa habari kamanda wa Polisi Mkoa huo, Awadh Jum Haji leo Febuari 08, ofisini kwake Mwembe Madema amesema watuhumiwa hao wamekamatwa jana Febuari, 7 saa 02:45 Usiku maeneo ya Shakani katika Ufukwe wa bahari Wilaya ya Magharib B’ Unguja.

Kamanda Awadh amesema askari wakiwa doria katika maeneo hayo walikamta gari yenye namba za usajili namba Z 947 KQ aina ya Fuso ambayo ikiendeshwa na Salum Habuba Mohd (35) mkaazi wa Bububu. 
Amesema baada ya kufanya upekuzi katika gari hiyo walikuta maboksi 37 ndani yake yakiwa na simu za mkononi za aina mbalimbali, mfuko mmoja wa sukari kilo 50 na mashuka mawili ambavyo vilikuwa vinasafirishwa kwa njia ya magendo kwenda Tanzania Bara.
Amesema matukio hayo yanaikosesha Serikali mapato kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. 
Kamanda Awadh amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Yunus Hashim Ayoub (52), Salum Habuba Mohd (35), Khamis Haji Faki (35), Maulid Chambuso Mwinyi (29), Thomas Anton Lumumba (23), Juma Yahaya Issa (40), Suleiman Issa Hassan (32), Ally Juma Mussa (36) na Mohd Yunus Hashim (17).
Kamanda Awadh alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.