Profesa Janabi ataja walichobaini kwa watoto wenye uzito uliopitiliza

Muktasari:

  • Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imekamilisha sehemu ya kwanza ya uchunguzi. Awamu ya pili itaanza Septemba, 2024.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya watoto wenye uzito kupita kiasi, Imani Joseph (7) na Gloria Joseph (4) kuruhusiwa kurejea nyumbani, Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeeleza ilichobaini, ikisema inaingia hatua ya pili ya uchunguzi.

Akizungumza na Mwananchi Digital katika mahojiano jana Machi 21, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema wamemaliza hatua ya kwanza ya uchunguzi.

Watoto hao waliruhusiwa Machi 20, 2024 baada ya kukaa Mloganzila kwa siku 45 wakichukuliwa vipimo mbalimbali kubaini chanzo cha wao kuongezeka uzito kwa kasi na kuwaanzishia ‘diet’ (mpangilio maalum wa mlo).

Profesa Janabi amesema baada ya kuwapima vipimo vya lehemu, moyo, figo, kisukari na vingine kama vile CT Scan na MRI, hawajabainika kuwa na tatizo lolote kiafya.

“Tuliona ni jambo jema acha tusaidie hawa vijana, tulifanya utaratibu wa kwanza kupima vipimo, kitaalamu tulibaini hawana hitilafu mahali pengine popote, lakini mafuta yapo juu sababu ya uzito kuwa juu, hiki kitu kinaweza kuwa cha kuzaliwa nacho,” amesema.

Amesema kwa sasa wanaenda hatua ya pili kwa sababu wote wanapimwa kupitia gharama za Serikali, hakuna wanacholipa.

“Kuna wale ndugu wawili, kuna mama na baba kwa hiyo hii itakuwa hatua yetu ya pili kufanya uchunguzi, kwa sababu mwisho lazima kujua ni jeni gani ambayo imeleta hitilafu kubwa namna hii kwa mtoto wa miaka mitano kuwa na uzito wa kilo 61. Ni tatizo ambalo tunalifanyia uchunguzi, tukiweza kugundua kwanza itatusaidia kuelimisha hospitali  na taasisi nyingine, wazazi, ndugu na jamiii kwa ujumla,” amesema Profesa Janabi.

Amesema kwa kipindi chote cha matibabu ya watoto hao wamekuwa wakishirikiana na vituo vya kliniki za Lipid vya nchini Uingereza na Marekani na vingine vilivyopo Afrika.

Profesa Janabi amesema walikuwa wakifanya vipimo kuangalia uwezekano wa kuwawekea puto au kukata sehemu ya tumbo ili kuwapunguza unene.

Amesema walikuwa wanafanya mawasiliano na vituo vya nje, walibadilishana mawazo nini kinaweza kufanyika na kushauriana wazazi wapewe elimu ya lishe, jambo lililofanywa na wataalamu wa lishe.

“Tumeweza kuwapunguza uzito kidogo. Tumewarudisha Dodoma, kila mwezi watakuwa wanaonwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na katika kipindi hicho madaktari watakuwa wanawasiliana nasi katika miezi sita, baada ya hapo watarudi kwetu (Mloganzila) Septemba, 2014,” amesema.

Amesema wataangalia lishe kama imesaidia kufanya kazi kwa kuwa imeshawapa dalili nzuri.

“Tumerekebisha kwa sehemu kubwa milo ya watoto, walikuwa wanawapatia tu chakula, kwa hiyo tumewaelekeza vitu gani hasa vya kula. Chakula kimegawanyika sehemu tatu kubwa kuna protini, wanga na mafuta, moja kati ya mafundisho yetu mengi kwanza ni mpangilio wa chakula,” amesema.

“Mama tumempa maelekezo, chakula ambacho watoto wanakula ni vema wakaanza kula protini, chakula chenye mafuta na cha mwisho kiwe wanga, mboga za majani ziwe nyingi,” amesema.

Amesema wanga unapoliwa mwishoni husaidia kutumika kidogo kwa kuwa tayari vyakula vingine vinakuwa vimeshaliwa hivyo tumbo hujaa na kushiba.

Amesema wamewaanzishia tiba lishe kwa kuwa watoto hao bado wadogo, hivyo kuwaepusha na magonjwa yanayoweza kuwakumba kama vile ya figo, kisukari, moyo, shinikizo la juu la damu na pia matatizo ya afya ya akili.

Hata hivyo, Profesa Janabi hakuwa tayari kutaja uzito wa watoto hao kwa sasa akisema wanaendelea na tiba lishe.

Akizungumza na Mwananchi Digital baada ya kuruhusiwa, watoto hao, mama yao Vumilia Elisha alisema kwa kipindi chote walichokaa hospitalini, Imani na Gloria hawakuwahi kupewa dawa ya aina yoyote na wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Vumilia mkazi wa Mtaa wa Makole jijini Dodoma amesema: “Tulivyofika tulipokewa vizuri na watoto walianza kuchukuliwa vipimo vya awali na kila siku zilivyoenda waliendelea na vipimo mpaka tuliporuhusiwa.”

Januari 14, 2024 Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) kupitia gazeti la Mwananchi ilichapisha habari kuhusu uwepo wa watoto hao na Februari Mosi, Profesa Janabi alitoa nafasi ya matibabu bure kwa watoto hao, kupitia kliniki ya uchunguzi na matibabu ya ugonjwa unaosababishwa na wingi wa mafuta kwenye damu (Lipid clinic).

Watoto hao walifikishwa hospitalini hapo Februari 4, kwa msaada wa MCL iliyowasafirisha kutokea nyumbani kwao  Makole, Dodoma.

Baada ya vipimo Imani alikutwa na uzito wa kilo 76 na Gloria kilo 62.