VIDEO: Watoto waliopitiliza uzito watoka hospitali, mama asimulia matibabu yao

Muktasari:

  • Watoto waliokuwa na uzito uliopitiliza Imani Joseph (7) na mdogo wake Gloria Joseph (4) wameruhusiwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila baada ya kukaa kwa siku 45.

Dar es Salaam. Familia ya Joseph Kalenga na mkewe Vumilia Elisha sasa ina matumaini baada ya watoto wao, Imani (7) na Gloria Joseph (4) kuanza kupungua uzito mkubwa waliokuwa nao.

Na leo Jumatano Machi 20, 2024, watoto hao wameruhusiwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila walikokuwa wamelazwa.

Januari 14, mwaka huu, gazeti la Mwananchi lilichapisha habari kuhusu hali ya watoto hao na baadaye Februari mosi, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi alitoa nafasi ya matibabu bure kwao, kupitia kliniki ya uchunguzi na matibabu ya ugonjwa unaosababishwa na wingi wa mafuta kwenye damu.

Watoto hao walifikishwa hospitalini hapo Februari 4, mwaka huu kwa msaada wa Mwananchi iliyowasafirisha kutokea nyumbani kwao Kata ya Makole jijini Dodoma na baada ya vipimo, Imani alikutwa na uzito wa kilo 76 na Gloria kilo 62.

Mloganzila imetumia siku 45 kuchukua vipimo mbalimbali ili kubaini chanzo cha watoto hao kuongezeka uzito kwa kasi na kuwaanzishia mpangilio wa mlo kamili..

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Machi 20, 2024, mama wa watoto hao, Vumilia amesema kwa kipindi chote walichokaa hospitalini hapo, Imani na Gloria hawakuwahi kupewa dawa ya aina yoyote, bali walipatiwa tiba lishe iliyowasaidia kupungua kwa kiasi kikubwa.

Watoto waliopitiliza uzito watoka hospitali, mama asimulia matibabu yao

Mama huyo mkazi wa Mtaa wa Makole jijini Dodoma, amesema tangu alipofika wamepimwa vipimo mbalimbali pamoja na vile vikubwa vilivyohusisha moyo, kichwa na mifupa.


Mpangilio wa chakula

Akielezea lishe waliyoipata ikiambatana na mafunzo kwa mama ya namna ya kuwaandalia mlo, Vumilia amesema maisha kwa watoto hao yalikuwa mazuri na chakula pia kilikuwa kizuri.

Kwa kuwa watoto hao awali walikuwa wanakula wali au ugali kilo tano kwa wakati mmoja, amesema kutokana na mtiririko wa chakula walichokuwa wamepangiwa kukitumia, kilikuwa ni kizuri na haikuleta shida sana kwa sababu hawakuchukua muda mrefu kukizoea.

Vumilia amesema wanawe walipangiwa nini wale asubuhi, mchana na jioni.

“Kila siku walipewa kitu tofauti. Kuna nyakati walikuwa wanakunywa chai ya maziwa kikombe kimoja wanapewa na kipande cha kiazi na yai moja la kuchemsha. Mchana ilitegemea kuna nyakati ugali kiasi kidogo kutokana na wao wenyewe jinsi walivyo na umri wao, mbonga za majani na nyama ya kuku au kipande cha samaki,” amesema.

Mama huyo amesema jioni walikuwa wanakula tambi inaweza ikawekwa na nyama, njegere na mboga za majani kwa wingi.

Vumilia amesema licha ya kwamba watoto wake walizoea kula chakula kingi, haikuwachukua muda waliridhika na kile walichopangiwa.

“Haikuwachukua muda waliwahi kuridhika, kwa kuwa zile mbogamboga za majani zilikuwa zinawekwa kwa wingi, kama ni njegere hivyohivyo, kwa hiyo hata kama tambi zinawekwa kidogo, wanashiba na hawakuwahi kusumbua,” amesema.

Hata hivyo, Vumilia amesema changamoto kubwa inayomkabili kwa sasa ni uwezekano wa kuendelea na lishe waliyopangiwa kutokana na hali yake ya uchumi.

“Vyakula vyote walivyokuwa wanakula hospitali Dodoma pia vinapatikana, lakini vyote vinapatikana kwa kununua, uwezekano wa kuvipata vyote kwa mtiririko kama huku walivyokuwa wanavipata ni kwa kiasi kidogo sana kwa uwezo wangu,” amesema.

Mama huyo amesema anatamani watoto wake waendelee kupata mlo kamili kama ilivyokuwa hospitalini kwa sababu umewasaidia wamepungua uzito.

“Nimeridhika. Hii imenionyesha hata nilipofika hapa stendi (Mbezi –Magufuli), siku wanakuja changamoto ilikuwa kubwa kwa sababu mdogo alikuwa hawezi kabisa hata kunyanyua mguu mpaka apate msaada, tofauti na leo mkubwa ameweza kupanda mwenyewe kwenye basi bila usaidizi na mdogo anajitahidi ingawaje tumemsaidia kupanda, kuna tofauti kubwa,” amesema.

Akizungumzia suala la kuushughulisha mwili, Vumilia amesema watoto hao kwa siku zote walizokuwa hospitali, walikuwa wakifanya mazoezi kupitia vifaa vya wagonjwa vilivyokuwepo hospitalini hapo.

Hata hivyo, watoto hao wanaondoka hospitalini kwa masharti maalumu ambayo mama huyo amesema wataalamu wa afya hasa daktari wa lishe aliyekuwa akiwasimamia, ameagiza.

“Nimesisitizwa kwenye mlo, nizingatie ili waendelea kupungua uzito, kwenye suala la kurudi (hospitali) wameniambia, ila ni kwa mwezi wa tisa (Septemba), ninaweza kurudi lakini hawajaniacha hivihivi.

“Katikati hapa wameniunganisha na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma, watakuwa wakiwafutilia watoto kwa ukaribu na kujua wanaendeleaje,” amesema.

Vumilia amesema majibu ya watoto hao yametoka na watayaweka hadharani madaktari, lakini yeye ameambiwa watoto hawana tatizo lolote, hivyo amepangiwa namna watakavyohudhuria kliniki.

Mama huyo ambaye kwa mara ya kwanza aliandikwa na gazeti la Mwananchi, ametoa shukrani zake kwa uongozi, wadau mbalimbali waliowezesha pamoja na Hospitali ya Mloganzila.

“Ninamshukuru sana Mkurugenzi Profesa Janabi kwa maana amenisaidia kuondoa ile hofu niliyokuwa nayo kama mzazi, nilikuwa natamani kujua shida ni nini inayosababisha watoto wangu waongezeke uzito kwa kasi, amenisaidia sana.

“Madaktari wote walikuwa pamoja na mimi nawashukuru sana, wengine walikuwa wanacheza na watoto wangu, walifurahia uwepo wao,” amesema Vumilia.