Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Lipumba anena na vijana miswada Sheria za Uchaguzi

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasi Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na vijana, wakati akifungua kongamano la vijana linalolenga kujadili miswada mitatu ya Sheria za Uchaguzi leo Jumanne Desemba 19, 2023 jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Vijana watakiwa kushiriki mijadala kuboresha miswada Sheria za Uchaguzi.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba amewataka vijana kuipitia na kuijadili miswada mitatu ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni.

 Hatua hiyo amesema itawawezesha kutoa mapendekezo yatakayowezesha sheria kuwa na tija kwa vijana.

Amesema mjadala unawezesha kutibu kasoro zilizojitokeza kwenye chaguzi zilizopita, ukiwamo wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Profesa Lipumba ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Desemba 19, 2023 alipofungua kongamano la vijana linalojadili Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa. Miswada hiyo iliwasilishwa bungeni Novemba 10, 2023.

“Kongamamo hili la mitazamo ya vijana kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi limekuja wakati mwafaka kwa vijana waliopo kwenye vyama vya siasa, kujikita kutoa hamasa na elimu kwa vijana wenzao ili waipitie na kuisoma miswada hii na kujiandaa kushiriki katika chaguzi zinazokuja,” amesema.

Profesa Lipumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), amesema iwapo Rais Samia Suluhu Hassan atasimamia kikamilifu na kwa weledi mabadiliko ya sheria mbalimbali zinazolalamikiwa na wadau wote wakakubaliana na mabadiliko hayo, atajenga imani kubwa ndani na nje ya nchi na atatuma ujumbe utakaoacha alama kwenye jumuiya za kimataifa.

“Endapo, Rais Samia Suluhu Hassan atafanikisha suala hilo na kutekeleza kwa vitendo falsafa yake 4R aliyoianzisha, historia yake haitafutika kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke ambaye atakuwa ameongoza mabadiliko ya kisheria na kikatiba,” amesema.

Balozi wa Uholanzi nchini, Wiebe de Boer, amesema Waholanzi wanathamini mchango wa vijana katika demokrasia ndiyo maana wameamua kuifadhili TCD ili kuwaita vijana na kuwapa fursa ya kufanya mijadala kuhusu sheria za uchaguzi.

“Niwaombe viongozi vijana waliopo kwenye vyama vya siasa wahakikishe wanatumia vyema fursa waliyonayo kupigania masilahi ya vijana wenzao kwenye masuala mbalimbali yanaowahusu kwa kuwa vijana ndiyo nguvukazi, hivyo wanatakiwa kujadili miswada hii kwa masilahi mazuri ya Taifa,” amesema.

Mwanaharakati wa Katiba, Deus Kibamba, amesema katika miswada hiyo kuna mambo mazuri ambayo yamezingatiwa, akitoa mfano wa muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2023 umewekwa takwa la lazima kwa vyama vya siasa kuwa na sera za masuala ya kijinsia ambayo baadhi ya vyama havina.

Amesema pia muswada huo umeweka takwa la lazima kwa vyama vya siasa kuhakikisha nyaraka zake za ndani zinazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Kibamba amesema Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023 unapendekeza uwepo wa waratibu wa uchaguzi katika kila mkoa.

“Sheria hii ikipitishwa itasidia kuondoa kasoro zilizokuwa zinajitokeza kipindi cha uchaguzi,” amesema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana ya CUF (Juvi-CUF), Zanzibar, Khadija Abdillatif amesema kuna haja kwa Serikali ya Tanzania Bara, kutekeleza takwa la kuanzishwa kwa Baraza la Vijana ili wapate jukwaa halisi watakalokutana, kujadiliana na kutoa maamuzi ya pamoja.

“Tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetekeleza takwa hilo kwa muda mrefu na linafanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo sioni ugumu unaosababisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushindwa kutekeleza hilo kama ina lengo la kuwatumia vijana kikamilifu,” amesema.

Mratibu wa Uhamasisha wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Taifa, Twaha Abdallah amewataka vijana kupitia miswada hiyo na kutoa maoni ili iweze kuboreshwa kabla ya kusainiwa na Rais na kuwa sheria rasmi.

Katika mdahalo huo, uliandaliwa na TCD kwa ufadhili wa ubalozi wa Uholanzi nchini, umeshirikisha vijana kutoka vyama Chadema, CCM, ACT- Wazalendo, NCCR-Mageuzi, Chama cha Ukombozi wa Umma, CUF na mtandao wa asasi za kiraia.