Lissu, Mbowe, kigogo wa CCM waichambua miswada ya uchaguzi
Muktasari:
- Wadau wa masuala ya sheria na siasa wamejadili miswada ya Sheria za Uchaguzi, huku wakibainisha upungufu na kutoa mapendekezo ya kuboresha ili kukidhi mahitaji, wawakilishi wa CCM na Chadema wapendekeza miswada hiyo iondolewe bungeni, ikafanyiwe marekebisho.
Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Mohamed Said Mohamed ameungana na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)-Bara, Tundu Lissu kupendekeza miswada ya Sheria za Uchaguzi iondewe bungeni na kufanyiwa marekebisho.
Wametoa mapendekezo hayo leo Ijumaa, Desemba 15, 2023 wakati wakichangia mada kwenye kongamano la wadau kujadili miswada hiyo, lililoandaliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Miswada hiyo iliyojadiliwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa vyama vya siasa, mawakili, asasi za kiraia ni Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Akichangia mada katika kongamano hilo, Lissu amesema miswada hiyo haijabainisha tatizo la mfumo wa uchaguzi nchini na akahoji kama tatizo hilo linaweza kutibiwa na vifungu vinavyopendekezwa katika miswada hiyo.
Amesema katika muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, mambo mapya yaliyojitokeza ni kuunganisha tu sheria mbili tofauti, yaani Sheria ya Uchaguzi wa Rais na Madiwani na Sheri ya Uchaguzi wa Madiwani na kuwa moja na jambo la pili ni mgombea anapokuwa mmoja kupigiwa kura ya ndio au hapana.
Katika Muswada wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Lissu amesema jambo pekee jipya linalopendekezwa ni kamati ya usaili ambayo pia amesema kuwa ni ya Rais kama ilivyo wakurugenzi na akahoji kama hilo ndilo tatizo la kimsingi la Tume ya Uchaguzi ya Tanzania.
Akichambua matatizo ya mfumo wa uchaguzi, Lissu amesema tatizo la kwanza ni usimamizi, akisema hilo limekuwa likibainishwa na waangalizi wa uchaguzi tangu mwaka 1995.
Lissua amesema tatizo la pili ni usajili wa wapigakura akisema udhibiti wake unafanywa kwa siri na kwamba tatizo la tatu ni uteuzi wa wagombea hasa wa upinzani wamekuwa wakienguliwa na la nne ni kampeni akidai zimekuwa ni vurugu tu.
Pia, Lissu amesema tatizo la tano ni maadili na la sita ni mawakala wa usimamizi na saba akidai siku ya uchaguzi hakuna udhibiti wa nani anaingia kwenye kituo na matokeo yatangazwaje.
"Haya yamezungumzwa miaka yote na watazamaji wa uchaguzi wetu. Kwa hiyo hii miswada iondolewe ikaandikwe upya ili ijibu matatizo ya uchaguzi wetu," amesema Lissu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar, Mohamed amesema anaunga mkono kwamba kumekuwa na kukurupuka kipindi cha uchaguzi, hivyo wanataka kufanya marekebisho yote.
"Pia naungana mkono Tundu Lissu, miswada hii iondoshwe mpaka baada ya uchaguzi ndio ifanyiwe kazi pamoja na marekebisho ya Katiba maana muda uliopo ni mfupi. Hivyo tuiondoe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu, ili twende sambamba na mabadiliko ya Katiba yetu," amesema Said.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema miswada hiyo ili iwe na mantiki na kufanya kazi, ni lazima kuwepo na mabadiliko hata madogo ya Katiba yatakayozingatia hayo mapendekezo.
Amependekeza marekebisho ya Katiba yahusu Tume Huru, mgombea binafsi na uwiano wa 50 kwa 50, huku akisema kwa muda uliobakia haiwezekani kufanya mabadiliko ya Katiba yote.
"Mwenyekiti na makamu wa tume pia waende kwenye usaili, ili Rais asiteue tu watu anaowataka," amesema Profesa Lipumba akianisha mapendekezo kwenye miswada hiyo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema ili kuisaidia nchi wasifanye utani kwenye suala la uchaguzi.
Amesema Rais aliunda Kikosi Kazi kikahoji wadau mbalimbali na kutoka na mapendekezo mbalimbali na kwamba wao pia walifanya maridhiano na CCM kwa mwaka mzima, lakini tatizo ni dhamira ya CCM ya kufanya mabadiliko haipo.
"Haiwezekani tukawapelekea mapendekezo kwa miswada ambayo imeshasomwa, tunatarajia wayafanyie kazi. Huu ni utani unaofanywa na CCM haina dhamira ya mabadiliko.
"Tulifungua kesi Mahakama ya Afrika Mashariki tukisema Sheria ya Vyama vya Siasa inakiuka hata Itifaki ya Afrika Mashariki na Mahakama imaamua Serikali ifanye marekebisho, lakini Serikali haijazingatia uamuzi huo wa Mahakama ya Afrika Mashariki," amesema Mbowe.
Awali, akifungua kongamano hilo, Rais wa TLS, Harold Sungusia amesema kwa asilimia kubwa mapendekezo yao huwa hayafanyiwi kazi.
Ametoa mfano sheria iliyopitishwa hivi karibuni ya marekebisho ya Sheria ya TLS walipendekeza muda wa urais ni mfupi hautoshi, lakini Serikali ikaweka mambo mengine mengi.
"Kwa hiyo tunapeleka mapendekezo, halafu yanakuja na mambo ambayo hamjayapendekeza," amesema Sungusia.
Hata hivyo, amesema katika miswada hiyo mitatu wana uwezo wa kupeleka mapendekezo yaliyo bora.
"Kwa hiyo katika kongamano kama hili tunapojadili pamoja tunaweza kupeleka mapendekezo bora, ndio maana tumeona badala ya kujifungia wenyewe tu tuwashirikishe nanyi," amesema.
Wachokoza mada katika kongamano hilo walikuwa Deus Kibamba na Dk Idd Mandi ambao walichambua vifungu mbalimbali wakionyesha upungufu na mapendekezo wanayopendekeza yaingizwe katika miswada hiyo.