Profesa Mkenda aongeza muda zabuni

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ameagiza kuongezwa mwezi mmoja kwa muda wa kufungua zabuni lengo likiwa kupata washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ameagiza kuongezwa mwezi mmoja kwa muda wa kufungua zabuni lengo likiwa kupata washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Pia,  ameagiza tangazo la zabuni lipelekwe kwenye ofisi za Balozi za Tanzania kwenye nchi zinazozalisha mbolea duniani kupitia Wizara ya Mambo ya Nje.

Profesa Mkenda ametoa maagizo hayo jana baada ya kufanya ziara ya kikazi kwenye ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)  kwa ajili ya kuweka mikakati ili kuhakikisha mbolea bora inawafikia wakulima kwa wakati na bei nafuu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Juni 8, 2021 kwa niaba ya Profesa Mkenda, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TFRA, Profesa Anthony Mshandete amesema  muda wa kufungua zabuni ulikuwa unaisha Juni 18 lakini  umeongezwa hadi Julai 8, 2021.

 “Pia waziri ameagiza tangazo la zabuni lipelekwe kwenye balozi za nchi zinazozalisha mbolea zilizopo hapa nchini.  Pia TFRA iendelee na utaratibu wa kutangaza zabuni za BPS kwa kuwatumia wazabuni walioko kwenye kanzidata ya mamlaka ili kuhakikisha mbolea zinawasili nchini kwa wakati kwa msimu wa kilimo 2021/2022,” amesema.

Amesema Mkenda ameiagiza TFRA kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya mbolea nchini kwa kuwa fursa zipo nyingi ikiwa ni pamoja na utashi wa kisiasa, upatikanaji wa malighafi,  miundombinu rafiki, soko kubwa la mbolea ndani nan je ya nchi.