Putin anataka nini Ukraine?

Muktasari:

Kwa njia ya anga, nchi kavu na baharini, Alhamisi iliyopita Urusi ilianzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine, nchi ambayo ni ya kidemokrasia ya Ulaya yenye watu milioni 44 na vikosi vyake viko viungani mwa mji mkuu wa Kyiv.

Kwa njia ya anga, nchi kavu na baharini, Alhamisi iliyopita Urusi ilianzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine, nchi ambayo ni ya kidemokrasia ya Ulaya yenye watu milioni 44 na vikosi vyake viko viungani mwa mji mkuu wa Kyiv.

Kwa nini askari wa Urusi wameshambulia?

Wanajeshi wa Urusi wameukaribia mji mkuu wa Ukraine zikiwa ni siku chache baada ya kiongozi wa Urusi kuamuru uvamizi kamili kutoka kaskazini, mashariki na kusini. Katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya runinga kabla ya alfajiri Februari 24, Rais Putin alisema:

“Urusi haiwezi kujisikia salama kutokana na kuwapo na tishio la mara kwa mara Ukraine ya kisasa ... Urusi itajibu mara moja ikiwa jeshi lolote la nje litajaribu kuingilia kati ... Tuko tayari kwa matukio yoyote. Maamuzi yote muhimu yamefanywa katika suala hili. Natumai nitasikilizwa.”

Matamshi ya Putin yalikuja baada ya Marekani kusema Urusi imeweka takriban wanajeshi 150,000 karibu na mipaka ya Ukraine.

Putin alirejea malalamiko yake ya awali kuhusu kushindwa kwa Marekani na Jumuiya ya kujihami ya mataifa ya magharibi (Nato) kukidhi matakwa ya usalama ya Urusi.

Februari 22, 2014 Bunge la Ukraine lilipiga kura ya kumwondoa Rais Victor Yanukovych kwenye wadhifa wake ambaye aliungwa mkono na Urusi.

Baada ya kuondolewa, Urusi ililipiza kisasi kwa kuliteka eneo la kusini la Crimea na kuanzisha uasi mashariki mwa nchi hiyo, ikiwaunga mkono watu wanaotaka kujitenga ambao wamepigana na vikosi vya Ukraine.

Kwa muda mrefu Urusi imepinga hatua ya Ukraine kuelekea Umoja wa Ulaya na Nato. Akitangaza uvamizi wa Urusi, Putin aliishutumu Nato kwa kutishia “mustakabali wetu wa kihistoria kama Taifa”.

Hata hivyo, Urusi na Ukraine hazijawa na uhusiano rasmi wa kidiplomasia tangu Februari 24, mwaka huu. Shirikisho la Urusi na Ukraine kwa sasa ziko katika vita. Ingawa uvamizi wa Urusi kwa Ukraine umeanza mwezi huu, ukweli ni kwamba vita na tetesi za vita vilianza mwaka 2014 baada ya Urusi kuinyakua Crimea kutoka Ukraine.

Baada ya Muungano wa Kisovieti kusambaratika Desemba 1991, uhusiano wa kimataifa kati ya nchi hizo mbili umepitia vipindi vya mivutano na uadui. Mwanzoni mwa miaka ya 1990, sera ya Ukraine ilitawaliwa na matamanio ya kuhakikisha mamlaka na uhuru wake, ikifuatiwa na sera ya kigeni iliyosawazisha ushirikiano na Umoja wa Ulaya, Urusi, na sera nyingine zenye nguvu.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa wa uhasama tangu kufanyika kwa kile kilichoitwa ‘Mapinduzi ya Utu’ mwaka 2014, ambayo yalimwondoa madarakani Rais Yanukovych na wafuasi wake kwa sababu alikataa kutia saini mkataba wa chama cha kisiasa na biashara huria na Umoja wa Ulaya (EU) ambao uliungwa mkono na wengi katika Bunge la Ukraine.

Baada ya mapinduzi hayo, Serikali mpya ya Ukraine ilitaka kuuweka mustakabali wa nchi hiyo ndani ya Umoja wa Ulaya na Nato, badala ya kuendelea kucheza mchezo wa kidiplomasia wa kusawazisha maslahi yake ya kiuchumi na kiusalama na yale ya Urusi, EU, na wanachama wa Nato.

Mwaka 2004 Jamhuri ya Czech, Estonia, Hungaria, Latvia, Lithuania, Poland na Slovakia zilijiunga na EU, ikifuatiwa na Bulgaria na Romania mwaka 2007.

Kwa kutazama hatua zote hizi, Serikali ya Urusi ilihofia uanachama wa Ukraine katika Umoja wa Ulaya na Nato ungekamilisha ukuta wa magharibi wa nchi washirika kwa kuizuia Urusi kuingia katika Bahari Nyeusi.

Huku Korea Kusini na Japan zikiwa washirika wa Marekani, Serikali ya Urusi ilikuwa na wasiwasi kwamba Urusi ilikuwa inazungukwa na kuzingirwa na mataifa yenye uhasama.

Kutokana na hayo ‘Mapinduzi ya Utu’, Urusi iliwaunga mkono wanamgambo wanaotaka kujitenga katika Jamhuri ya watu wa Donetsk na Jamhuri ya watu wa Luhansk katika vita kwenye eneo muhimu kiuchumi la Donbas la Ukraine, kwenye mpaka wake wa mashariki na Urusi.

Eneo hili lina watu wengi wa kabila la Kirusi. Hadi mwanzoni mwa mwaka huu, vita hiyo ilikuwa imeshaua zaidi ya watu 13,000, na kusababisha vikwazo vya nchi za magharibi dhidi ya Urusi.

Mwaka 2019, marekebisho yalifanywa kwa Katiba ya Ukraine ambayo ilisisitiza kutobadili mikakati yake kama nchi kuelekea uanachama wa EU na Nato.

Katika kipindi chote cha mwaka 2021 na 2022, jeshi la Urusi kwenye mpaka wa Ukraine lilizidisha mvutano kati ya nchi hizo mbili na kudhoofisha uhusiano, huku Marekani ikituma ujumbe kwamba uvamizi huo ungekabiliwa na matokeo mabaya kwa uchumi wa Urusi.

Pamoja na yote hayo, Alfajiri ya Februari 24, mwaka huu Urusi ilivamia Ukraine, jambo lililoifanya Ukraine kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Urusi.

Je! Urusi itaenda umbali gani katika vita hii?