Raia wa kigeni jela kuingia nchini bila vibali

Muktasari:
- Raia wawili wa Burundi na Malawi wameshindwa kulipa faini ya Sh2.5 milioni hivyo wameenda kutumikia kifungo cha miaka miwili jela.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu raia wawili wa Burundi na Malawi kulipa faini ya Sh2.5 milioni au kwenda miaka miwili jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu likiwemo la kuingia nchini bila kibali.
Waliohukumiwa ni raia wa Burundi, Omary Hezemunyano (25) na Godbless kandawile (27) wa Malawi.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na shtaka la kuingia na kuishi nchini bila kibali pamoja na kutoa taarifa za uongo Ili wapatiwe kitambulisho cha taifa.
Shaidi amesema mshtakiwa Hezemunyano ametiwa hatiani kwa makosa matatu hivyo anatakiwa kila kosa moja kulipa Sh500,000 ambapo jumla ni Sh1.5 milioni huku Mkandawile ametiwa hatiani kwa makosa mawili kila moja anatakiwa kulipa sh 500,000 hivyo jumla atalipa Sh1 milioni.
"Washtakiwa hawa wamekiri makosa yao hivyo wanatakiwa kulipa faini wakishindwa wataenda kutumikia kifungo cha miaka miwili jela," amesema Shaidi.
Hata hivyo washtakiwa hao wameenda kutumikia kifungo cha miaka miwili jela baada kishindwa kulipa faini hiyo
Awali, Wakili wa Serikali, Hadija Masoud aliwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao kwa pamoja siku na mahala pasipojulikana waliingia nchini bila kibali au nyaraka yoyote iliyowaruhusu kuingia ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alidai Oktoba 13, 2023 washtakiwa hao wakiwa katika ofisi za Uhamiaji jijini Dar es Salaam walikutwa wakiwa nchini bila kibali.
Masoud amedai mshitakiwa Hezemunyano
aitoa taarifa za uongo ili kujipatia kitambulisho cha Taifa chenye majina ya Omary Martin.
Amedai kuwa Oktoba 13, 2023 washtakiwa wote walikamatwa na maofisa wa uhamiaji na kuhojiwa ambapo walikiri kutenda makosa hayo.
Washtakiwa wote walipoulizwa na Hakimu kuhusu maelezo hayo walikuri kutenda makosa hayo.
"Hawana kumbukumbu ya makosa ya jinai kwa washtakiwa hao hivyo naiomba mahakama hii kuwapa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hii," amedai Masoud.