Rais Magufuli amteua Kichere kuwa CAG

Muktasari:

  • Charles Kichere aliwahi kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Magufuli ambaye alimteua tena kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Juni 8, mwaka huu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Novemba 3, 2019 amemteua Charles Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Uteuzi huo unaanza kesho, Kichere anachukua nafasi ya Profesa Mussa Assad ambaye kipindi chake cha uongozi cha miaka mitano kinaishia kesho.

Mteule huyo ambaye alikuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alitenguliwa uteuzi wake na Rais Magufuli ambaye alimteua tena kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Juni 8, mwaka huu.

Akisoma taarifa ya uteuzi huo leo Jumapili Novemba 3, 2019, Balozi John Kijazi amesema nafasi ya Kichere itajazwa na Katarina Revocati ambaye alikuwa Msajili Mkuu wa Mahakama.

Pia, Rais Magufuli amewateua Aisha Amour kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Kanali Francis Mbindi kuwa kamishna wa kazi ofisi ya Waziri Mkuu na majaji 12 wa Mahakama Kuu.

SOMA ZAIDI HAPA