CAG abaki na mshangao Dodoma

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, alipokuwa akitoa ripoti za ukaguzi kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2018. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amesema licha ya kuwaalika wabunge katika mkutano wake akieleza taarifa yake ya ukaguzi inayoishia Juni, 2018 hawakuja, hajui sababu za kutofika katika mkutano huo.

Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)), Profesa Mussa Assad amesema hajui sababu za wabunge, hasa wenyeviti wa kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Serikali za Mitaa kutoshiriki mkutano wake na wanahabari wakati akieleza taarifa za ukaguzi wa ofisi yake mwaka unaoishia Juni, 2018.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika ofsi yake jijini Dodoma tofauti na miaka mingine ambapo hufanyika katika ukumbi wa habari wa Bunge, Profesa Assad amesema, “kuna wanahabari hapa hawakuja na hamuulizi kwa nini hawakuja, kuna wenyeviti hawakuja hapa, sijui kwanini hawakuja ila (wabunge) nitawapa nakala ya mazungumzo yetu na watayatumia.”

“Hili jambo kuwa tunafanyia mkutano hapa (katika ofisi za CAG) si la kukurupuka na tulilifikiria muda mrefu na tuliwahi kusema mwaka huu tutafanya mkutano ofisini kwetu, tukasema kwa mambo yalivyo tunaweza tusikaribishwe ndani ya Bunge, huenda hata mwakani tukafanyia hapa.”