Rais Magufuli apigilia msumari wa mwisho ujenzi Bandari ya Bagamoyo

Rais wa Tanzania John Magufuli

Muktasari:

Rais John Magufuli amesema masharti magumu yaliyowekwa na wawekezaji waliokuwa wanataka kujenga Bandari ya Bagamoyo ndio chanzo cha kutokujengwa mpaka sasa.


Wakati Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ukiwa umegubikwa na maswali mengi yaliyokosa majibu hatimaye Rais wa Tanzania John Magufuli ameweka wazi kwa nini ujenzi huo haujafanyika huku akisema masharti magumu ya wawekezaji hao ndiyo sababu kubwa ya mkwamo huo.

Ameeleza kuwa masharti ambayo yalitolewa na wawekezaji hao ni magumu na kichaa pekee ndiye anaweza kuyakubali.

Rais Magufuli alitoa ufafanuzi huo jana wakati wa kikao maalum kilichomkutanisha na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Tanzania nzima Ikulu Jijini Dar es salaam.

Miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na kuwa baada ya ujenzi huo wa bandari hiyo,  Tanzania haitaruhusiwa  kujenga na kuendeleza bandari nyingine yoyote kuanzia Tanga mpaka Mtwara.

Pia alisema wawekezaji hao walitaka wakishajenga bandari hiyo Tanzania isiruhusiwe kukusanya kodi katika bandari hiyo.

“Wanataka ukishawapa pale huruhusiwi hata kwenda kukusanya kodi.  TRA mnayoisema hapa hairuhusiwi kukanyaga pale wakishafanya uwekezaji,” alieleza Rais Magufuli.

Rais Maguguli alisema pia sharti lingine katika mkataba wa Ujenzi wa Bandari hiyo ya Bagamoyo ni kuwa wanatakiwa kupewa muda wa miaka 33 bila kuwauliza chochote watakapokuwa wamewekeza hapo, pamoja na kuwalipa wale watakaokuwa wanafanya kazi ya kuchimba hiyo bandari.

Rais Magufuli aliwaeleza wafanyabiashara kuwa masharti hayo ni magumu na yalikuwa na lengo la kuua bandari nyingine za Tanzania ambazo zinaendelezwa huku akisema Serikali ilifanya utafiti wa kutosha na kuona uwekezaji huo hautakuwa na tija kwa Taifa zaidi ya kuwaumiza Watanzania.

Sakata la kusimama ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo liliibuliwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai katika Bunge la Bajeti baada ya wabunge mbalimbali kuihoji serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu suala hilo ambapo Spika Ndugai aliitaka serikali kueleza kwa nini ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo umesimama huku akieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kungekuwa na faida kwa Taifa.

Spika Ndugai alilieleza Bunge kuwa kwa kutizama umuhimu wa bandari hiyo ni zaidi ya miradi mingine inayoendeshwa na serikali kama Reli ya kisasa, hivyo ni muhimu kuwa na bandari hiyo kwanza.

Katika bunge hilo Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi,  Isack Kamwelwe alisema majadiliano kati ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika ujenzi huo na serikali yanaendelea na pindi yatakapomalizika ujenzi huo utaendelea.