Rais Magufuli awazungumzia wapinzani kujitoa uchaguzi serikali za mitaa

Muktasari:

Uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Tanzania ulifanyika Jumapili iliyopita Novemba 24, 2019 ambapo vyama vya upinzani sita vilisusia kushiriki uchaguzi huo.

Shinyanga. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema kitendo cha vyama vya upinzani kususia uchaguzi wa serikali za mitaa ni demokrasia huku akisisitiza kuwa maendeleo hayana chama na Watanzania wanatakiwa kutanguliza mbele maslahi ya Taifa.

Hii ni kauli ya kwanza kutolewa na Rais Magufuli tangu baadhi ya vyama vya upinzani kumwomba kuingilia kati madai yao ya wagombea wao kutokutendewa haki wakati wa shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita Novemba 24, 2019.

Katika uchaguzi huo, vyama vya siasa vya Chadema, ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Mageuzi, UPDP na Chaumma ambapo CCM kimeshinda vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.9, mitaa 4263 sawa na asilimia 100 na vitongoji 63,970 sawa na asilimia 99.4.

Leo Jumatano Novemba 27, 2019,  akizungumza na wananchi wa Isaka wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Rais Magufuli ameyasema amekipongeza Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ushindi katika uchaguzi huo.

“Nawashukuru sana ndugu zangu wa Isaka mmemaliza chaguzi, nimeambiwa Chama Cha Mapinduzi kimepasua vizuri. Hongereni sana, maendeleo ndugu zangu hayana chama na demokrasia hata kujitoa nayo ni demokrasia, kususia uchaguzi nayo ni demokrasia,” amesema Rais Magufuli.

 “Kwa hiyo nawapongeza kwa ushindi mkubwa mlioupata chama cha mapinduzi lakini maendeleo hayana chama ni lazima tushikamane wote kujenga taifa letu, tunachohitaji ni maendeleo, ukileta maji, wote watakunywa, uwe CCM, uwe Chadema, ukileta bandari hapa kila mmoja atafanya biashara,” amesema

Hata hivyo, aliwaomba Watanzania watangulize mbele maslahi ya Taifa wawe wamoja ili waweze kujenga nchi ya Tanzania