Rais Mwinyi aagiza manispaa kupunguza kodi

Pemba. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amuagiza uongozi wa manispaa na mabara ya miji Mkoa wa Kusini Pemba, kuhakikisha wanasimamia mwenendo wa wafanyabiashara na kupunguza kiwango kikubwa cha kodi ili waweze kupata kipato na kukuza biashara zao.
Dk Mwinyi aliyasema hayo leo Novemba Mosi, 2023 wakati akizungumza na wananchi na watendaji wa umma katika hafla ufunguaji wa jengo la wajariamali Michakaini katika Mji wa Chake Chake.
Alisema Baraza la Manispaa Halmashauri na Mabara ya Miji ndio yenye jukumu la kusimamia mwenendo wa wafanyabiasha katika kuona wafanyabiashara wanafanya shughuli zao kwa ubora.
Alisema haiwezekana kuona mabaraza yanatoa kodi kubwa ambayo itamfanya mfanyabiashara kushinda kulipa kodi kutokana kiwango kikubwa kilichowekwa na taasisi hizo.
Alisema jambo jengine ni kusimamia kuona wafanyabiashara wote wanatumia maeneo ya ndani ya soko na sio wengine wawepo nje wengine ndani huo itakuwa sio utaratibu nzuri wa kuendesha biashara.
Aidha alisema kuwepo kwa mazingira bora ya uwendeshaji na utunzaji wa biashara kati ya mabaraza ya Manispaa itaongeza ukuaji wa biashara na wajasiriamali wataweza kupiga hatua kuchumi.
‘’Mabaraza la Miji na Manispaa nyinyi ndio wenye jukumu la kusimamia katika mambo mbali mbali ikiwemo kodi na kutumika kwa maeneo maalumu yaliyotengwa kufanyia biashara na sio wale wapo ndani wengine wapo nje huo sio utakuwa sio utaratibu nzuri’’alisema Dk Mwinyi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais tawala za Mikoa na idara Maalum za Smz, Issa Makhodhu Haji alisema kufunguliwa kwa kituo hicho kitasaidia kukifungua Kisiwa cha Pemba kiuchumi.
Aidha alisema jengo hilo limegharimu zaidi ya Sh7 bilioni ambapo kujengwa kwake kutaondosha changamoto ya wafanyabiashara ya kukosa maeneo ya kuendeshea shughuli zao.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Matar Zahor Massoud alisema kituo hicho kimejengwa kufuatia ahadi za Rais kwa wajasiriamali kuweza kupata maeneo salama ya kuuzia na kuhifadhia bidhaa zao wakati akigombea kuwa Rais wa Zanzibar.