Rais Mwinyi abainisha uimarishaji viwanja vya ndege kuongeza watalii Z’bar

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali imeboresha sekta ya utalii kwa kutumia miundombinu ya kisasa ya utoaji huduma bora kupitia viwanja vya ndege vya Zanzibar na kuwavutia watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali.

Rais Mwinyi ameyasema hayo leo Aprili 6, 2023 alipozungumza na Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Peter Huyghebaert, alipofika Ikulu Zanzibar kujitambulisha.

Amemueleza balozi huyo kwamba utalii ndio sekta mama ya uchumi kisiwani humo ikihusisha na sekta zingine za uwekezaji kupitia sera yake ya uchumi wa buluu.

“Zanzibar tuna safari za ndege za moja kwa moja kutoka Ubegiji, hali hii pia imeongeza watalii wengi kutoka huko, tunaamini idadi itaongezeka zaidi kutokana uhusiano mzuri baina yetu,” amesema Dk Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema uhusiano uliopo baina ya Ubelgiji na Tanzania ikiwemo Zanzibar kumekuwa na urafiki mzuri baina yao kwani nchi imekuwa ikipokea watalii wengi kutoka nchini humo.

Akizungumzia sekta ya afya, Dk Mwinyi amemueleza balozi huyo kuangalia uwezekano wa kuimarisha ushirikiano zaidi kwenye sekta hiyo hasa masuala ya Tehama ambako eneo hilo lina uhitaji zaidi wa kuongeza ujuzi na kubadilishana uzoefu kwa wafanyakazi.


Naye bolozi Peter Huyghebaert, amesema urafiki wa diplomasia uliopo baina ya Ubelgiji na Tanzania ikiwemo Zanzibar anaamini utaendelea kuzaa matunda mazuri yatakayowanufaisha wananchi wa pande zote mbili.

Balozi huyo amemuahidi Rais Mwinyi kwamba wataendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuimarisha matumizi ya teknolojia hasa kwenye sekta ya afya.

Tanzania na Ubelgiji zimekua na uhusiano wa diplomasia na biashara  tangu miaka ya 1980 ambapo kwa mara ya kwanza Ubelgiji ilifungua ubalozi wake Dar es Salaam mwaka huo na Tanzania ilifungua ubalozi wake mji mkuu wa nchi hiyo, Brussels.