Rais Mwinyi akoshwa makusanyo ya kodi, aagiza ZRA waongezwe mishahara

Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi akimkabidhi tuzo Rashid Ali aliyekuwa mhamasihaji bora kulipa kodi kudai na kutoa risiti za kielektroniki

Muktasari:

  • Ampa ‘tano’ Kamishna Mkuu wa ZRA, Yusuph Mwenda kwa ubunifu, mwenyewe asema Zanzibar ina mfumo wa kodi rafiki

Unguja. Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi amesema anaridhishwa na mabadiliko yanayofanywa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), yanayosaidia kuongeza makusanyo na kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.

Rais Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Desemba 29, 30 katika kilele cha mwezi wa shukrani na furaha kwa walipa kodi, kusema kwa kipindi kifupi ZRA imeleta mabadiliko makubwa ya kikodi Zanzibar.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Kamishna Mkuu wa ZRA, Yusuph Mwenda kuwa mbunifu na kuleta mabadiliko ya kiutendaji, uongozi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

“Nimekuwa nikisema hapa kama mtu akifanya vibaya mseme hadharani, lakini akifanya vizuri pia mseme hadharani, nikupongeze na watendaji wako haya mapato tunayoyapata kama sio mabadiliko ZRA tusingeyapata,” amesema Rais Mwinyi.

Amesema katika kipindi cha miezi mitano katika mwaka wa fedha 2023/24; ZRA ilipangiwa kukusanya Sh276 bilioni, lakini imekusanya Sh565 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 104.

Amesema kwa kipindi kirefu Zanzibar ilikuwa haitekelezi miradi mikubwa kama ambavyo inatekelezwa sasa ikiwemo miradi ya ya maji, barabara, afya, elimu na viwanja vya michezo, na kwamba hayo yote yanafanyika hayo kwa sababu ya ufanisi katika ukusanyaji mapato pamoja na  matumizi sahihi ya fedha hizo.

Hivyo, Rais Mwinyi ameigiza Wizara Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, kufanya marekebisho ya mishahara ya wafanyakazi wa ZRA, ili kuangalia upya maslahi yao.

Mbali na maslahi, pia Rais Mwinyi ameagiza kuhakikisha katika bajeti ya Serikali ZRA inapata asilimia 100.

“Taasisi inayokuongezea mapato kwa asilimia 51 kwa miezi mitano hatuna budi na sisi kuwaangalia kwa namna ya pekee, ukitaka fedha lazima utumie fedha, kwa hiyo hili ni agizo ambalo sitegemei lishindwe kutekelezwa,” amesema Rais Mwinyi.

Hata hivyo, amewataka baadhi ya watendaji wa mamlaka hiyo wanaoshirikiana na wafanyabiashara kutaka kukwepa kodi, waache mara moja na iwapo wakibainika hatua zaidi zitachukuliwa.

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kuwekeza Zanzibar, akisema Serikali itaendelea kurahisha mazingira ya biashara na ulipaji kodi.

Kamishana Mkuu wa ZRA, Yusuph Mwenda amesema mazingira mazuri na mifumo iliyowekwa imesaidia kuongezeka kwa ulipaji kodi wa hiari na kuongeza makusanyo ambapo kodi imekuwa kwa asilimia 51.

Amesema hatua hiyo inaonyesha mafanikio makubwa kwa sababu kwa kawaida ukuaji wa kodi katika nchi za Afrika ni asilimia 20.

Amesema makusanyo kwa mwaka 2021, ZRA ilikusanya Sh374 bilioni, lakini kwa mwaka 2023 wamekusanya Sh565 bilioni.

“Zanzibar ina mfumo wa kodi rafiki unaorahisisha biashara, maana unajenga usawa hakuna ambaye anapendelewa au anaonewa kulipa kodi, kwa hiyo unarashisha ulipaji kodi wa hiari,” amesema Mwenda.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema katika bajeti ya Serikali ya mwaka jana ilikuwa na utegemezi wa asilimia 26, lakini kwa mwaka ujao wa fedha wamepunguza utegemezi hadi kufika asilimia mbili kutokana na ongezeko la makusanyo ya ndani.

Katika kilele hicho, ZRA imetoa tuzo na vyeti kwa wafanyabiashara waliofanya vizuri kwa kipindi cha mwaka mzima.