Rais Mwinyi: Zanzibar inahitaji kuzalisha umeme wake yenyewe

Dk Mwinyi akiwa kwenye mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya WAPCOS Limited ya nchini India.
Muktasari:
- Kwa sasa Zanzibar inapokea megawati 110 za nishati ya umeme kutoka Tanzania Bara kupitia baharini.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji uwekezaji mkubwa katika sekta za maji na umeme ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hizo.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 7, 2024 ikulu mjini Unguja katika mazungumzo yake na uongozi wa Kampuni ya WAPCOS Limited ya nchini India.
Amesema kwa sasa Zanzibar inapokea megawati 110 za nishati ya umeme kutoka Tanzania Bara kupitia baharini.
“Serikali ina dhamira ya kuzalisha umeme wake yenyewe na iko tayari kushirikiana na kampuni yoyote itakayokuwa tayari ili kuanza hatua za upembuzi yakinifu,” amesema.
Pia, Dk Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji utafiti wa kina wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati hizo kwa kuangalia zaidi uwekezaji na huduma za uhakika.
Kwa mantiki hiyo, Dk Mwinyi ameikaribisha kampuni ya WAPCOS Limited kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika sekta hiyo.
Amesema, SMZ na India ni washirika wakubwa kwenye huduma za jamii na nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu.
Naye Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya WAPCOS Limited, Rajni Kant Agrawal amesema kampuni yao imejikita zaidi na kutoa huduma za ushauri hususani kwenye nishati za umeme, maji na miundombinu.
Amesema wapo tayari kushirikiana na SMZ kwenye uwekezaji wa sekta hizo.
Amesema, kwa Tanzania Bara tayari kampuni hiyo inafanya kazi maeneo ya Dar es Salaam, Bagamoyo na maeneo mengine ya nchi ikiwemo Zanzibar.