Rais Ramaphosa atua DRC ziara ya siku mbili

Muktasari:

  • Rais wa Afrika Kusini Ramaphosa awasili nchini DRC katika kuhakikisha anaboresha mahusiano ya nchi zao kwa kuzungumzia mambo ya usalama na biashara katika nchi hizo.

Kongo. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amewasili jijini Kinshasa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ziara rasmi ya siku mbili ambapo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Felix Tshisekedi.

Kiongozi huyo wa Afrika Kusini anatarajiwa kukutana na Tshisekedi katika Palais de la Nation, makao rasmi ya Rais mjini Kinshasa ambapo watapata chakula cha mchana na kujadili mambo mbalimbali yanayohusisha nchi zao huku wakilenga kuboresha mahusiano ya nchi hizo mbili.

Ajenda kuu katika mazungumzo yao wanatarajia kuzungumzia mambo ya usalama na biashara. Ziara hiyo imekuja wakati Kinshasa inajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu huku kukiwa na matatizo ya usalama nyumbani, mashariki mwa nchi.

Kwa mujibu wa kituo cha habari ‘The EastAfrican’ wameeleza kwamba pande hizo mbili hivi majuzi zilianzisha tena Tume Kuu ya Pamoja ya DRC na Afrika Kusini siku ya Jumanne, ambapo mawaziri wakuu kutoka pande zote mbili wanatarajiwa kufanya kazi ya kurekebisha mikataba baina ya nchi hizo mbili.

Naibu Waziri Mkuu anayeshughulikia Mambo ya Nje, Christophe Lutundula amesema tume ya pamoja itaimarisha uhusiano kati ya Afrika Kusini na DR Congo.

“Afŕika Kusini daima imekuwa na DRC. Tunayofuraha kukumbuka wakati mwafaka wa mikutano hii, ambayo itaimarisha ushirikiano kati ya nchi zetu mbili. Siku za hivi karibuni Afrika Kusini imekuwa upande wa Malawi na nchi nyingine za SADC kusaidia DRC kuondokana na makundi yenye silaha,” ameeleza.

Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Thandi Ruth Modise aliwasili Kinshasa siku ya Jumatatu kabla ya safari ya Ramaphosa, kuashiria ushirikiano wa usalama. Alikuwa akiongoza tume ya usalama ya tume ya pamoja ya DRC na Jamhuri ya Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa programu rasmi, Marais Cyril Ramaphosa na Félix Tshisekedi watashiriki leo Alhamisi katika kongamano la kiuchumi la DRC na Afrika Kusini.