Rais Samia aagiza uchunguzi kuungua Soko la Kariakoo

Gesi KariaKoo yazuia wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao

Muktasari:

Rais Samia  pia ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martin Shigella na Jumuiya za Kiislamu Tanzania  kufuatia kuungua moto kwa Bweni la Shule ya Sekondari ya Kiislam ya Wasichana  At  Town

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto uliotokea usiku wa jana katika Soko la Kariakoo jijini hapa.

Rais Samia ameeleza kuwa soko hilo lina mkusanyiko mkubwa wa wafanyabiashara na kuteketea kwa soko hilo kutakuwa kumesababisha hasara kubwa kwa wapangaji na wamiliki wa soko hilo kongwe nchini.

 Katika taarifa yake iliyotolewa leo Julai 11 2021 na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Samia amesema Soko la Kariakoo licha ya kuajiri wafanyabiashara wengi lakini ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo tukio hilo si hasara kwa Wafanyabiashara tu bali hata kwa Serikali.

Sambamba na maelekezo hayo ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla na wafanyabiashara wa soko hilo kufuatia hasara kubwa waliyoipata.

 Rais Samia  pia ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martin Shigella na Jumuiya za Kiislamu Tanzania  kufuatia kuungua moto kwa Bweni la Shule ya Sekondari ya Kiislam ya Wasichana  At  Town inayomilikiwa na Taasisi ya Kiislamu iliyopo  mji Mpya katika Manispaa ya Morogoro.

 Amesema kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kuungua moto kwa shule zinazomilikiwa na Jumuiya za Dini nchini hivyo ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na  Jumuiya hizo kutafuta vyanzo vya matukio hayo na kuyadhibiti ili matukio ya kuungua moto kwa shule hizo yasijirudie.