Rais Samia achangia Sh150 milioni KKKT Hai
Muktasari:
- Ni kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Nshara Machame, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Hai. Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa Sh150 milioni kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Nshara Machame, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Mbowe ambaye anasali katika kanisa hilo, leo Jumapili Desemba 31, 2023 ameongoza harambee hiyo ambapo zaidi ya Sh800 milioni zimepatikana zikiwemo ahadi na fedha taslimu.
Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dk Fredrick Shoo aliongoza ibada iliyoenda sambamba na harambee hiyo.
Akizungumza kwenye harambee hiyo Mbowe amesema hakuna sababu ya itikadi za kisiasa kuwatenganisha Watanzania katika shughuli za kijamii.
“Sisi sote ni wamoja, maendeleo yanapopatikana kila mmoja wetu ananufaika nayo, hizi shughuli za kusaidia jamii hazipaswi kututenganisha kisiasa” amesema.
Mbali na Rais Samia kutoa mchango huo, pia Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa amechangia Sh10 milioni na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amechangia Sh10 milioni katika ujenzi huo.
"Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa ameshatoa Sh10 milioni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama Samia (Samia Suluhu Hassan) na familia yake wametoa Sh150 milioni na wameshaweka kwenye akaunti ya Kanisa," amesema Mbowe.
Mbowe amesema wamepokea michango kutoka kwa mawaziri, wabunge na wafanyabiashara ambao hawakufanikiwa kushiriki ibada hiyo ya harambee.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria harambee hiyo ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amir Mkalipa, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe, Halima Mdee na Ester Bulaya.