Rais Samia agusa maisha ya diwani mwenye ulemavu
Muktasari:
Ampatia kiti mwendo cha kisasa chenye thamani ya zaidi ya Sh3.1 milioni.
Same. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kiti mwendo cha kisasa chenye thamani ya zaidi ya Sh3.1 milioni kwa diwani wa viti maalum mwenye ulemavu Jamila Mdee (28) wa wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro.
Diwani huyo aliyepata ulemavu baada ya kuanguka sakafuni na kuvunjika uti wa mgongo mwaka 2008, amekabidhiwa kiti mwendo hicho kinachotumia umeme na Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni kwa niaba ya Rais Samia.
Neema hiyo imemshukia diwani huyo baada ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda kufanya ziara wilayani humo, Januari 22 na kumuahidi diwani huyo kupatiwa kiti mwendo hicho, baada ya kuwasilisha kero yake kwa kiongozi huyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Same mjini.
Akizungumza wakati akikabidhi kiti hicho jana, Januari 26 Mkuu wa wilaya hiyo, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiti hicho akisema kitamsaidia kwenda kusikiliza kero za wananchi kwa kutekeleza ilani ya CCM.
"Hiki kiti kimeletwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amemuagiza Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda kwamba ni lazima hiki kiti apewe, kwa hiyo Makonda ametekeleza kama Rais alivyomuagiza," amesema Mgeni.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa kiti hicho, Jamila alimshukuru Makonda na Rais Samia kwa kuyagusa maisha yake na kwamba ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu kupata kiti cha namna hiyo.
"Namshukuru Rais Samia kwa kunigusa maisha yangu ilikuwa ni kiu yangu sana kukipata hiki kiti, namshukuru Mungu amefanya wepesi nikapata hiki kiti kwa uharaka zaidi, sifa na utukufu ni kwa Mwenyezi Mungu,"
Mwaka 2008 Jamila akiwa darasa la sita alianguka sakafuni na kuvunjika uti wa mgongo na kupata ulemavu wa kudumu.
Hakukata tamaa baada ya kupata changamoto hiyo na baadaye aliingia kwenye masuala ya siasa na mwaka 2020, ambapo kwa sasa ni diwani wa viti maalum.