Watu wenye ulemavu Geita wapewa viti mwendo 55
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Terry Strong (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe (kulia) wakiwasukuma baadhi ya walemavu walionufaika na viti mwendo vilivyotolewa na kampuni hiyo kwa ushirikiano na Shirika la CCBRT.
Muktasari:
- Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Hospitali ya CCBRT wametoa viti mwendo na vifaa saidizi 55 kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Geita. Watu wenye ulemavu mkoani Geita wamepewa msaada wa viti mwendo na saidizi 55 kutoka Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Hospitali ya CCBRT.
Msaada huo umekabidhiwa jana Jumatano, Novemba 22, 2023 Mjini Geita kupitia mpango maalumu wa usambazaji viti mwendo, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao mbalimbali.
Mkuu wa wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya makabidhiano hayo, amewapongeza GGML kwa kuendelea kuijali jamii ya watu wanaouzunguka mgodi huo.
Pia, ameipongeza CCBRT kwa kuungana na GGML kutoa elimu ya kitaalamu kuhusu matumizi sahihi na kutoa ushauri sahihi wa vifaa hivyo vya watu wenye ulamvu.
“GGML wamekuwa washirika wakubwa wa shughuli za maendeleo, wamefanya mambo mengi na mazuri kwa manufaa ya wananchi na wanaoishi katika mkoa huu, tunawashukuru sana,” amesema.
Ameahidi Serikali kuendelea kuunga mkono wawekezaji ikiwamo GGML ambayo ni kampuni inayoungana na jamii kutoa vitu na misaada ya utu kwa watu wenye mahitaji mbalimbali.
Mmoja wa wanufaika wa msaada huo, Matendo Sitta amesema,“Tunaomba msiishie kwetu kwa sababu kuna wenzetu wengi wenye changamoto, hivyo tunaomba waendelee kuwa na moyo wa utoaji kwa sababu sasa hivi tunaweza kwenda hata kwa jirani na tunaahidi kutunza vyombo hivi.”
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong amesema kampuni hiyo imejitolea kuendelea kuzingatia utu kwa watu wote ikiwamo wadau wetu na jamii tunayofanyia kazi.
“Huu ni miongoni mwa mipango kadhaa ya huduma za afya ambayo tumeifanya kwa ushirikiano na CCBRT ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa bidii katika kutoa huduma za matibabu na urekebishaji wa viungo mbalimbali vya mwili kwa gharama nafuu na kuwawezesha watu wenye mahitaji maalumu na familia zao kurejesha tabasamu.
“Tunaamini kila mtu anastahili utu, heshima na fursa sawa za kustawi maishani. Pia tunatambua watu wanaoishi na ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi na vikwazo katika kupata huduma za msingi, elimu, ajira na ushirikishwaji wa kijamii. Ndiyo maana tunajivunia kuunga mkono mpango huu ambao utawapa huduma zinazofaa na zilizoboreshwa ambazo zitaboresha uhuru na ubora wa maisha,” amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa CCBRT, Dk Neophita Lukiringi amewashukuru GGML kwa kuwafikiria watu wenye ulemavu na kuwapatia viti mwendo ambavyo ni sahihi.
Amesema mtu mwenye ulemavu akipatiwa kiti mwendo ambacho si sahihi, kinaweza kumletea madhara zaidi.
“GGML waliona pamoja na kuwasaidia watu wenye ulemavu hawakutaka kugawa hovyo hovyo, wakafikiria tupate vifaa ambavyo vitawasaidia kweli. Kwa hiyo, napenda kuwashuruku kwa kuonyesha mfano mzuri, kwani mtu mwenye ulemavu ukimpatia kiti mwendo sahihi utakuwa umemsaidia sana,” amesema.
Amesema mtu mwenye ulevu akipatiwa kiti mwendo kisicho sahihi kinaweza kumsababisha apinde mgongo, kifupishe misuli yake na kumuongezea ulemavu zaidi.
“Kama amechukua kiti mwendo ambacho si sahihi utamfanya apate vidonda mgandamizo ambavyo vinachukua muda mrefu sana kupona na wakati mwingine vinasambaza wadudu kwenye mfumo wa damu mwisho wanakufa kabla ya wakati.
“Nasisitiza GGML wamefanya jambo zuri kutoa msaada sahihi ambao hautawaongezea ulemavu watu wenye ulemavu, pia utawasaidia watoto kwenda shule na kushiriki kucheza na wenzao huku watu wazima nao wakishiriki shughuli mbalimbali za kijamii,” amesema.
Ametoa wito kwa Watanzania wanaopenda kusaidia watu wenye ulemavu wasitoe viti mwendo bila kutafuta watalaamu wa kushirikiana nao kwa sababu hata Shirika la Afya Duniani (WHO) linasisitiza viti mwendo vitolewe na watu waliofunzwa, ili kukabili madhara hayo.