Rais Samia ahoji sababu ukosefu wa maadili kwa vijana

Saturday October 02 2021
samiapic

Rais Samia Suluhu Hassan

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam.  Rais  Samia Suluhu Hassan amehoji sababu ya ukosefu wa maadili kwa vijana licha kuwapo Chama cha Skauti, Girl Guides na Umoja wa Vijana wa vyama vya siasa.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 2, 2021 kwenye Siku ya Mlezi wa Skauti Tanzania inayofanyika jijini Dodoma na kuzitaka taasisi hizo kujiuliza wanakwama wapi.

Amesema licha ya kuwepo kwa mfumo mkubwa kwa taasisi hizo wa ufanyaji shughuli zake, bado kumeendelea kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili kwa vijana.

Amesema ukiangalia mfumo wa Skauti ni mkubwa na  unaendana na wa Serikali.

“Lakini Tanzania tujiulize, ukiangalia mfumo wa Skauti, mfumo wa vijana wa umoja wa Chama cha Mapinduzi, Umoja wa Vijana wa vyama mbalimbali vya siasa na Girl guides wetu, tujiulize ukosefu wa maadili, vitendo viovu unatoka wapi Tanzania.

“Tukiwa tuna taasisi zote hizi zenye mifumo mikubwa lakini bado tuna idadi kubwa ya vijana wanaopotoka,tujiulize tunakwama wapi, tumekosea wapi na hilo swali naliacha kwa taasisi  zote nilizozitaja hapa,”amesema Rais Samia.

Advertisement

Soma zaidi:Skauti waomba kurudishwa katika bajeti ya Serikali

Katika hatua nyingine, Rais ameahidi kuziunganisha taasisi za Girl guides na Skauti na kueleza kuwa amebaini kuna umbali kati yao licha ya kwamba wanafanya kazi zinazofanana.

“Kama nilivyosema nilikuwa kiongozi wa Girl guides sasa nitawaunganisha vema na Skauti kwa sababu nilivyokuwa mlezi wa Girl guides niliona kuna ‘gape’ kati yao kwani wakati wote kazi ni ileile isipokuwa Girl guides imejielekeza zaidi kwa watoto wa kike huku skauti ikichukua wote.

“Hivyo kuna kinyang’anyiro cha majukumu hapa, itabidi tukae pamoja tuziangalie ili zote ziende vizuri,’ amesema.

Advertisement