Rais Samia aisuka upya Tanesco

Rais Samia aisuka upya Tanesco

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemteua aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Miradi (PDB), Omari Issa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme (Tanesco).


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemteua aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Miradi (PDB), Omari Issa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme (Tanesco).

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Jaffar Haniu leo Jumamosi Septemba 25, 2021 imesema pia Rais amemteua aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika Mashariki na Magharibi wa Multichoice Afrika, Maharage Chande kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco.

“Chande anachukua nafasi ya Dk Tito Mwinuka.”

Taarifa hiyo pia imemtaja aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Shirika la Kusafisha Mafuta (Tipper), Michael Minja ambaye sasa ameteuliwa kuwa Kamishna wa Petrol na Gesi, Wizara ya Nishati.

“Amemteua Felschemi Mramba kuwa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu. Kabla ya uteuzi huu Mramba alikuwa Mshauri Mkuu wa Kiufundi chuo cha ufundi cha Tanesco.

“Amemteua Bw. Hassan Seif Said kuwa Mkurugenzi Mkuu, Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Kabla ya uteuzi huu, Seif alikuwa Meneja wa Kanda Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki Tanesco. Anachukua nafasi ya Bw. Amos Maganga,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema uteuzi huu umeanza tarehe  Septemba 23, 2021.

Wakati huohuo, taarifa hiyo imesema Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga amewahamisha Watumishi Waandamizi watano kutoka Tanesco kwenda Ofisi ya Rais, Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambako watapangiwa kazi nyingine.

Watumishi hao ni pamoja na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uwekezaji, Mhandisi Khalid James, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji na Masoko Mhandisi Raymond Seya, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usafirishaji Mhandisi Isaac Chanje, aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi Nyelu Mwamaja na Amos Ndegi aliyekuwa Mwanasheria wa Tanesco.