Rais Samia anavyotumia mitandao ya kijamii
Muktasari:
- Wakati hotuba zake zikiendelea kuleta matumaini mapya kwa Watanzania, Mwananchi limebaini Rais Samia Suluhu Hassan ni mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii ya Twitter na Instagram.
Dar es Salaam. Wakati hotuba zake zikiendelea kuleta matumaini mapya kwa Watanzania, Mwananchi limebaini Rais Samia Suluhu Hassan ni mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii ya Twitter na Instagram.
Rais Samia amekuwa akiandika katika mitandao hiyo mambo aliyoyafanya kwa siku husika au kuwatakia heri Watanzania au kutoa pole kwa mambo tofauti yanayotokea, jambo linalomuweka karibu na wananchi.
Watanzania nao wamekuwa wakiandika kwenye ukurasa wake wakieleza walivyo na matumaini na uongozi wake, miongoni mwao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye jana aliandika kwa hisia kuonyesha matumaini yake, huku akimwomba awapatie Katiba mpya.
Juzi, Rais Samia aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akiwatakia Watanzania Sikukuu njema ya Pasaka na kuwataka kuliombea Taifa, kudumisha amani na kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa.
“Nawatakia Watanzania wote Pasaka njema, tuadhimishe ufufuko wa Yesu Kristo huku tukiliombea Taifa letu la Tanzania kudumisha amani, upendo na mshikamano. Tuendeleze jitihada za kuijenga nchi yetu kwa kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa. Yesu amefufuka, Haleluya Haleluya,” ameandika Rais Samia.
Katika ujumbe huo, Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe aliandika maoni yake: “Mama Samia, nimejitahidi kubana hisia zangu kwa muda, nimeshawishika kukushukuru kwa kututakia kheri ya Pasaka sisi wakristo. Jamii ya Chadema tunashukuru ila napenda kutoa ombi la Pasaka ‘Tupatie Katiba mpya’. Usiku mwema mama, Mheshimiwa Rais.”
Vilevile, mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameandika katika ukurasa wa Rais Samia: “Upendo huunganisha Taifa. Asante kwa upendo wako kwa watu wako. Mapumziko mema ya Pasaka pia!”
Aprili Mosi, Rais Samia pia aliandika kuhusu kuwaapisha mawaziri na manaibu waziri katika mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri aliyoyafanya. Siku hiyo, aliweka pia vipande vifupi vya video kutoka kwenye hotuba aliyoitoa akisisitiza ushirikiano baina ya viongozi wa Serikali.
Katika ujumbe huo, mwanaharakati, Onesmo Olengurumwa aliandika: “Siyo Serikali tu iwe na ushirikiano, bali Taifa zima tuwe wamoja na tushirikiane kujenga Taifa. Taifa lilikuwa limegawanyika na kuna watu walijiona wao ndio wenye haki kuliko Watanzania wengine. Naamini wewe utatuleta pamoja tushirikiane tujenge Taifa kwa pamoja.”
Machi 28, Rais Samia aliandika kwamba alipokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru). Maneno yake yaliambatana na kipande cha video kinachomwonyesha akitoa maelekezo.
“Leo nimepokea taarifa za mwaka wa Fedha 2019/2020 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Nimeagiza kufanyiwa kazi na kuchukuliwa hatua mara moja kwa ushauri na dosari zote zilizoainishwa katika taarifa hizo,” aliandika Rais Samia.
Machi 26, ilikuwa siku ambayo Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli alizikwa na Rais Samia aliandika Tweet zaidi ya tano kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza akitoa shukrani kwa wananchi pamoja na wakuu wa nchi mbalimbali.
Kabla ya hapo, Machi 18, Rais Samia aliweka kipande cha video kinachomwonyesha akitangaza kifo cha Hayati Magufuli kilichotokea Machi 17 kikiwa kimeambatana na maneno: “Taarifa ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Mambo ambayo amekuwa akiyaandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, amekuwa akiweka pia kwenye mtandao wa Instagram. Hata hivyo, katika mtandao wa Instagram, tukio la mwisho aliloandika ni lile la kuapisha mawaziri, Aprili Mosi.
Akizungumzia Rais Samia kutumia mitandao ya kijamii, mchambuzi wa siasa, Andrew Bomani alisema inampa nafasi ya kupata mrejesho kutoka kwa wananchi kuhusu mambo ambayo Serikali yake inayafanya.
“Nadhani ni jambo zuri, Rais anapata feedback (mrejesho) kutoka kwa wananchi wake na hiyo inampa nafasi ya kujua namna uamuzi wake ulivyopokelewa na wananchi,” alisema.