Rais Samia asaini muswada Bima ya Afya kwa Wote

Muktasari:

  • Mwezi mmoja baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Rais Samia Suluhu Hassan ameitia saini na kuwa sheria kamili.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametia saini muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote na sasa imekua sheria kamili.

Novemba 2, 2023 Bunge lilipitisha muswada huo kwa asilimia 100 na kuweka historia, baada ya mkwamo uliokuwepo kwa takribani miaka mitano tangu ulipofufuliwa upya mwaka 2018.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya jana Desemba 4, 2023 imesema muswada huo sasa umeshasainiwa na Rais na kuwa sheria kamili, baada ya kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Desemba Mosi, 2023.

Saini ya Rais katika sheria hiyo, inaipa kazi Wizara ya Afya kuanza utungaji wa kanuni kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa sheria hiyo, ambayo itawezesha kila Mtanzania kupata huduma za afya pasipo na kikwazo cha kiuchumi.

Katika kufanikisha hayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi iliweka msisitizo wa umuhimu wa kuwa na mfuko kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo, na Serikali iusimamie kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya.

Kupitia sheria hiyo kutakuwa na utaratibu wa utambuzi na usajili wa kundi la watu wasio na uwezo, kwa lengo la kuhakikisha wanapata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.

Kundi hilo litajumuishwa kwenye skimu ya Bima ya Afya ya Umma kwa namna itakavyoainishwa kwenye kanuni zitakazotungwa hapo baadaye, huku akibainisha vyanzo vya mapato vitakavyotumika kugharamia skimu hiyo.

Akiusoma muswada huo bungeni kwa mara ya mwisho, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema vyanzo vya mapato ya skimu hiyo ni pamoja na sehemu ya mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa.

"Kwenye vinywaji vyenye kaboni, vinywaji vikali, bidhaa za vipodozi, kodi ya michezo ya kubahatisha, ada ya bima za vyombo vya moto na mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki " alisema Waziri Ummy.

Aliuhakikishia umma juu ya huduma za matibabu kwa kundi la wananchi wasio na uwezo.