Rais Samia ateua watatu, amtengua DED Sumbawanga
Muktasari:
- Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania imesema Rais Samia Suluhu Hassan ameteua viongozi mbalimbali na kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sumbawanga (DED).
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwapanga wasaidizi kwa kuteua watatu na kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sumbawanga (DED) mkoa wa Katavi, Catherine Masalla.
Taarifa ya uteuzi na utenguzi imetolewa usiku wa leo Alhamisi, Aprili 4, 2024 na Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu. Hata hivyo, haikuweka wazi sababu za Catherine kutenguliwa.
Katika uteuzi huo, Rais Samia amemteua Jaji Winfrida Kasoro kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria (LRCT). Jaji Karosso ni Jaji wa Mahakama ya Rufani.
pia, amemteua Alice Mtulo kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali. Kabla ya uteuzi huo, Alice alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Kesi na Udhibiti Ubora, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Mbali na hao, Rais Samia amemteua Bibiana Kileo kuwa Naibu Mkurugenzi Mashtaka katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mashtaka Mkoa (RPO) Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Mwanza.