Rais Samia awataka viongozi wa vyama vya siasa kuzika tofauti

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amesema kama kuna tofauti zozote walizonazo Watanzania ni wakati wa kuzizika na kufungua ukurasa mpya kama wamoja.


Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kama kuna tofauti zozote walizonazo Watanzania ni wakati wa kuzizika na kufungua ukurasa mpya kama wamoja.

Amesema hakuna sababu ya kutengeneza tofauti wakati watanzania ni wamoja na hakuna aliye bora mbele ya sheria.

Akizungumza leo Desemba 15 kwenye mkutano wa wadau wa kujadili hali ya demokrasi ya vya vyama vingi amesema kwa mamlaka aliyonayo ana jukumu la kuhakikisha amani na mshikamano vinatawala nchini.

“Niwaombe wenzangu wa vyama vya siasa mtambue kuwa kuelekezana, kuelimishana na kujadiliana ndiko kutakakoinusuru nchi yetu na majanga ya kisiasa na vurugu.

“Linapotokea jambo hatujakubaliana tukae, tuelimishane, tukubaliane, tuelekezane kama hatukukubaliana tutoke na msimamo wa kwamba nchi yetu ni taifa moja twende tukaimarishe demokrasia.

Amesema, “Kuna haja pia pale tusipokubaliana basi tupingane kwa hoja za kizalendo zenye kuongozwa na uhalisia wetu kiutamaduni, kiuchumi na kijamii.

 “Tuzungumze kufikia maridhiano ya kuzizika tofauti zetu, sisi ni taifa moja hakuna mwenye cheti cha kumiliki Tanzania wote tuna haki sawa,” amesema.