Rais Samia azindua mradi wa maji Mbalizi

Muktasari:

Mradi wa maji wa Shongo – Mbalizi utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 8 – 12 na utahudumia wananchi zaidi ya 80,000. Mradi huo utaongeza upatikanaji wa maji katika mkoa wa Mbeya kutoka asilimia 44 hadi asilimia 65.

Dar es Salaam. Rais wa Taznania, Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa maji wa Shongo – Mbalizi uliopo mkoani Mbeya ambao umegharimu zaidi ya Sh3.3 bilioni na utahudumia zaidi ya wakazi 80,000 katika eneo hilo.

Rais Samia ameanza ziara ya siku tatu mkoani Mbeya leo Ijumaa Agosti 5, 2022 ambapo atazindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo ikiwamo ya maji, afya, elimu na kilimo.

Akizungumzia mradi huo wa maji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Anthony Sanga amesema mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 8 – 12 na utahudumia wananchi zaidi ya 80,000.

“Mradi huu utaongeza upatikanaji wa maji katika mkoa wa Mbeya kutoka asilimia 44 zilizokuwepo kabla ya mradi huo hadi kufikia asilimia 65 za sasa baada ya mradi huo kukamilika,” amesema Sanga.

Akizungumza na wananchi wa Mbalizi, Rais Samia amewataka wananchi kuutunza mradi huo ili maji yaendelee kupatikana. Pia, amewataka watendaji wa taasisi za maji kuhakikisha maji yanapatikana kwa sababu serikali inatoa fedha nyingi kwenye miradi ya maji.

“Maji haya yamepatikana kwenye chanzo pale, ni matumaini yangu kwamba mtalinda kile chanzo. Ulinzi siyo jukumu letu, ni jukumu lenu wananchi. Mkiona watu wanaharibu chanzo kile, wawajibisheni kwa sheria mlizojiwekea.

“Niwaombe sana watendaji wa taasisi za maji, maji yasikosekane. Serikali inaweka fedha nyingi sana kuhakikisha maji yanapatikana. Kama maji yatakatika, toweni tangazo kwamba maji yatakatika pengine kwa sababu ya matengenezo,” amesema Rais Samia.

Amewataka wananchi kuendelea kufanya kazi ya uzalishaji kwa sababu serikali inakusanya mapato yake kutoka katika shughuli zao na fedha hizo ndiyo zinatumika kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Wananchi tuendeleze uzalishaji, mapato ya serikali yanatokana na uzalishaji wenu. Sisi serikali tunakusanya kodi na tozo kutokana na shughuli mnazozifanya. Na kodi hizo ndiyo zinaleta maji, barabara, umeme, afya na elimu,” amesema kiongozi huyo.

Awali, mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza alimtaka Rais Samia kuupandisha hadhi mji wa Mbalizi ili uwe halmashauri ya mji, jambo ambalo alisema litasaidia kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi.

Mbunge huyo amemshukuru Rais Samia kwa mradi huo wa maji pamoja na ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa hadi Mbalizi, akitaka barabara hiyo iongezwe kilomita mbili zinazosalia ili ifike uwanja wa ndege wa Songwe.