Rais Samia, Dk Steinmeier wakubaliana kukuza ushirikiano
Muktasari:
- Marais Samia Suluhu Hassan na Dk Frank Steinmeier wamefanya mazungumzo katika Ikulu jijini Dar es Salaam na kukubaliana kukuza na kuibua ushirikiano katika maeneo mapya.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Dk Frank Steinmeier wamekubaliana kukuza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili kwa manufaa ya wananchi wao.
Marais hao wameziagiza timu za watalaamu kuendelea na mazungumzo na mashauriano ya mara kwa mara yanayolenga kuboresha maeneo ya ushirikiano na kuibua na maeneo mengine mapya.
Rais Samia ameeleza hayo leo Jumanne Oktoba 31,2023 wakati akizungumza na wanahabari Ikulu Jijini Dar es Salaam, akiwa na Dk Steinmeier aliyewasili jana kwa ziara ya siku tatu nchini.
“Tumepata fursa ya kuzungumza masuala mengi muhimu yanayohusu Tanzania na Ujerumani, ikiwamo ushirikiano wa kijamii na kiuchumi. Uhusiano wa Tanzania na Ujerumani umefika miaka 60, katika kipindi chote tumekuwa tukishirikiana vema,” amesema Rais Samia.
“Serikali ya Ujerumani imekuwa rafiki, mshirika mzuri tulioshikana naye mikono katika sekta za afya, maji, kilimo, michezo na utamaduni, maliasili, ulinzi na elimu.”
Rais Samia amemhakikishia Dk Steinmeir kuwa Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mazungumzo yajayo ya ushirikiano wa maendeleo yatakayofanyika mwaka ujao.
Kuhusu biashara na uwekezaji, Rais Samia na mgeni wake walizungumzia na kusisitiza juu ya umuhimu wa mchango wa biashara na uwekezaji katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Tumekuwa na miradi isiyopungua 100 ya Ujerumani katika ngazi mbalimbali iliyowekezwa, lakini tumekuwa tukifanya biashara. Baadaye kutakuwa na kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Ujerumani litakalojadili fursa za uwekezaji,” amesema Rais Samia.
Mauzo ya biashara ya kutoka Tanzania kwenda Ujerumani kwa mwaka ni Dola 42.04 milioni za Marekani kwa bidhaa za kahawa, tumbaku, pamba na asali, samaki, nta na madini.
Rais Samia amesema Tanzania imekuwa ikipata utalii kutoka Ujerumani, na kuna uwezekano wa kuongeza zaidi baada ya kujitangaza vizuri katika Taifa hilo.
Rais Samia amesema mashirika ya Ujerumani yamekuwa yakisaidia uhifadhi wa mbuga za Selous na Serengeti.
Ujerumani ni miongoni wa nchi sita zinazoongoza kwa watalii nchini na mwaka huu Tanzania ilipokea watalii 67,718 kutoka Taifa hilo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, mgeni wake (Dk Steinmeier) ameipongeza Tanzania katika masuala ya demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, akisema imetulia katika maeneo hayo ndio maana wafanyabiashara wa Taifa lake wameshawishika kuja nchini kuangalia fursa.
“Ziara hii inathibitisha dhamira ya Serikali hizi mbili ya kuimarisha na kukuza ushirikiano na urafiki wetu kwa lengo la kuwanufaisha wananchi,” amesema Rais Samia.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Dk Steinmeier amesema Ujerumani itaendelea kuwa mshirika wa Tanzania katika maeneo mbalimbali.
Dk Steinmeier amesema ushirikiano huo utalenga zaidi maeneo ya nishati mbadala, kilimo na afya, akisema Taifa lake lipo tayari kusaidia elimu itakayoendana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Nilipokuja Tanzania kwa mara ya kwanza, nilivutiwa na vijana wabunifu, leo nataka nikawaone,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Steinmeier atawatembelea waathirika wa vita vya maji maji mkoani Ruvuma.
Vita hiyo iliongozwa na Kinjekitile Ngwale aliyenyongwa mwaka 1905.
Vita vya maji maji vilitokea kati ya mwaka 1905 hadi 1907. Inakadiriwa kuwa kati ya watu 180,000 hadi 300,000 walifariki dunia wakati wa vita hivyo huku sababu nyinginezo kama njaa na magonjwa zikitajwa kuchangia vifo hivyo.