Rais Samia, viongozi wa Afrika wamlilia Geingob

Muktasari:

  • Rais Hage Geingob wa Namibia amefariki dunia leo kwa maradhi ya saratani, alifanyiwa upasuaji mara kadhaa katika jitihada za kuokoa uhai wake.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine wa Afrika wametuma salamu za rambirambi kwa wananchi wa Namibia kufuatia kifo cha Rais wa nchi hiyo, Hage Geingob (82).

Geingob amefariki dunia mapema leo Jumapili, Februari 4, 2024 katika Hospitali ya Lady Pohamba iliyopo mji mkuu wa Windhoek alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Samia ameandika katika ukurasa wake wa X akisema: “Nimehuzunishwa sana na kifo cha Rais wa Namibia, Mheshimiwa Hage Geingob, ndugu mpendwa, mwanamajumui wa Afrika na rafiki mkubwa wa Tanzania.

“Kwa niaba ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natuma salamu za rambirambi kwa wananchi wa Jamhuri ya Namibia, Kaimu Rais, Mheshimiwa Dk Nangolo Mbumba, Mke wa Rais, Mheshimiwa Monica Kalondo, familia, marafiki na ndugu zangu wa SWAPO.

“Ninyi nyote mfarijike katika kipindi hiki kigumu. Roho yake ipumzike kwa amani. Amina.”

Kwa upande wake, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amenukuliwa na AFP akisema: “Leo, Afrika Kusini inaungana na watu wa nchi dada yetu ya Namibia kuomboleza kifo cha kiongozi, mzalendo na rafiki wa Afrika Kusini.

“Rais Geingob alikuwa mwanajeshi mkongwe wa ukombozi wa Namibia kutoka kwa ukoloni na ubaguzi wa rangi. Pia, alikuwa na ushawishi mkubwa katika mshikamano ambao watu wa Namibia waliutoa kwa watu wa Afrika Kusini, ili tuwe huru leo.”

Rais wa Kenya, William Ruto naye alirejea sifa hizo akisema: “Alikuwa muumini wa Afrika iliyoungana na alikuza sana sauti na mwonekano wa bara hili katika nyanja ya kimataifa.”

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Elias Magosi ameandika pia kwenye ukurasa wake wa X akisema:

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kusikitisha za kifo cha Hage Geingob, Rais wa Jamhuri ya Namibia asubuhi ya leo. Kwa niaba ya Sekretarieti ya SADC, tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa Serikali, familia ya wafiwa na watu wa Namibia kwa msiba huu mkubwa.”