RC Dar avitaka vituo vya afya kujifunza Aga Khan
Muktasari:
- Katika kufikia azma ya Serikali ya utalii wa matibabu, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Albert Chalamila amevitaka vituo vya afya kujifunza namna ya utoaji na uboreshaji huduma za afya, kupitia Hospitali ya Aga Khan (AKHA, T).
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amevitaka vituo vya afya vya umma kujifunza namna sahihi ya utoaji na uboreshaji wa huduma kupitia Taasisi ya utoaji huduma za afya Aga Khan, Tanzania (AKHA, T), ili kufikia azma ya utalii wa matibabu.
Chalamila ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2023 alipofanya ziara hospitalini hapo yenye lengo la kujadili hali ya afya katika mkoa na kuonyesha dhamira ya Serikali katika kuboresha huduma hizo nchini.
"Lazima tuige namna ambavyo wenzetu wanafanya tafiti zao na namna wanavyotafuta miradi mbalimbali ambayo wakiipata wanashirikiana na ili mjipanue zaidi, tunaona wanavyokabiliana na Uviko19 na magonjwa mengine, tunatakiwa kujifunza kutoka kwa Aga Khan ila huwezi kuomba hela kama hujawa na taasisi nzuri kiusimamizi," amesema Chalamila.
Amesema Aga Khan imeweza kushirikiana na Serikali, kufundisha wataalamu wa Amana na tayari wapo waliopata elimu.
"Wenzetu wameshapata elimu leo tuna furaha Amana ni kama Muhimbili na ICU ujenzi wake pale Aga Khan wamehusika kwa kiasi kikubwa na wakapeleka maarifa na ujuzi ili mitambo iliyofungwa ikafanye kazi isiharibike," amesema Chalamila.
Aidha Chalamila amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza utalii wa matibabu, na kwamba Serikali imeendelea kujenga zahanati na vituo vya afya na kuweka vifaa tiba vya kisasa na kwamba watumishi wanahitaji ujuzi na maarifa ya kuvitumia.
Ofisa Mtendaji Mkuu, Huduma za Afya Aga Khan, Tanzania Sisawo Konteh ameahidi kwamba wapo tayari kufanya kazi na vituo vyote vya afya vya umma na wanakaribisha kwa wale wanaotaka kujifunza kutoka kwao.
Awali Konteh alieleza malengo ya ziara ya RC huyo kuwa ni kushuhudia kituo cha kisasa cha matibabu na teknolojia na kushiriki katika kuimarisha mipango ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).
Amesema Chalamila kutizama maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Hospitali ya Aga Khan na Mamlaka za Mkoa wa Dar es Salaam ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma za afya katika mkoa huo.
Meneja wa mradi wa saratani, Dk Sara Maongezi amesema Aga Khan kupitia mradi huo wa miaka mitano wenye thamani ya euro milioni 13.3 sawa na Sh350.5 milioni wamefanya kwa kushirikiana na Serikali ambao ulitazamia kuwafikia wananchi milioni 1.7.
"Tulianza mradi kuhakikisha kila mdau yuko tayari na mradi huu unatekelezwa Dar es Salaam na Mwanza na tulifundisha watoa huduma 50 Mwanza na 50 Dar es Salaam jinsi ya kutambua saratani, namna ya upimaji na kutibu na pia tulitoa elimu kwa wanahabari na wahudumu wa afya ngazi ya jamii," amesema na kuongeza;
"Pia tuligawa mashine mbalimbali zinazotoa tiba kemia na vifaa vya upimaji hii inajumuisha pia ujenzi wa jengo la saratani ikiwa ni sehemu ya kushirikiana na Serikali."