RC Kilimanjaro ataka wananchi kushiriki kwa wingi Sensa
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kushiriki kwa wingi katika sensa ya watu na makazi na kusema mpaka sasa mwitikio wa wananchi waliojitokeza kuhesabiwa ni mkubwa.
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kushiriki kwa wingi katika sensa ya watu na makazi na kusema mpaka sasa mwitikio wa wananchi waliojitokeza kuhesabiwa ni mkubwa.
Babu ameyasema hayo leo Aprili 23, 2022 muda mfupi baada ya kuhesabiwa nyumbani kwake Shanti town, Manispaa ya Moshi.
"Wananchi wasisite kujitokeza kwa wingi na wale waliofichwa wajitokeze, mpaka sasa zoezi linaendelea vizuri na mwitikio wa watu ni mkubwa naamini mkoa wa Kilimanjaro utafanya vizuri zaidi kwa manufaa yetu," amesema Babu.
Ameongeza "Mimi tayari nimeshahesabiwa na karani ameniuliza maswali mazuri sana na imenichukua muda kama wa dakika kumi tuu,hivyo wananchi endeleeni kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa,"
Naye Mkuu wa wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutokuwa na hofu ya kuhesabiwa na kuwataka kutoa taarifa za kweli na zenye usahihi ili ziweze kusaidia serikali katika kutekeleza mipango yake.
"Lengo la kupata idadi ya Watanzania tuliopo ni ili mipango itakayopangwa ya kimaendeleo na serikali iendane na mahitaji halisi ya Watanzania," amesema Kayanda.