RC Mtambi: Eneo likiwa chafu, DC afike saa 12 asubuhi ofisini kwangu
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, operesheni hiyo itakuwa endelevu hadi pale viongozi watakapobadilika na kutekeleza wajibu wao ipasavyo
Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Kanali Evans Mtambi amesema kiongozi yeyote mkoani humo ambaye eneo analolisimamia litakutwa chafu, atalazimika kuripoti ofisini kwake saa 12 asubuhi kwa mazungumzo naye.
Kanali Mtambi amesema utaratibu huo unalenga kukomesha uchafu katika wilaya za mkoa huo, akisisitiza tayari Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Kaminyonge na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Tecla Mkuchika, wameshakumbana na hilo.
Akizungumza katika vikao tofauti vya mabaraza ya madiwani katika baadhi ya halmashauri za mkoa huo jana Juni 27, 2026, Kanali Mtambi amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mkoa unakuwa msafi.
Amesema ameamua kufanya vikao hivyo mapema asubuhi kabla ya muda wa kazi ili kuepuka kuingilia muda wa kuwahudumia wananchi kwa maelezo kuwa, vikao hivyo ni matokeo ya viongozi hao kushindwa kuwajibika.
"Siwezi kufanya tuition muda wa kazi, tutakuwa hatuwatendei haki wananchi ambao wanahitaji huduma yetu kwa muda huo.
“Badala yake kila kiongozi ambaye nitakuta uchafu katika eneo lake atalazimika kuja ofisini kwangu mapema sana bila kujali anatoka wilaya gani na kama hakutakuwa na mabadiliko hizi tuition tutazifanya hata usiku," amesema.
Amesema wakuu wa wilaya wataambatana na viongozi wa maeneo yaliyokutwa uchafu huo, wakiwamo watendaji wa kata, mitaa na vijiji.
Amesisitiza operesheni hiyo itakuwa endelevu hadi pale viongozi hao watakapobadilika na kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Amesema amebaini miongoni mwa sababu za kuwepo kwa uchafu katika maeneo mbalimbali mkoani humo ni kutokuwepo kwa kamati mbalimbali za kiuongozi zinazotakiwa kuwepo ngazi ya vijiji na mitaa.
Kanali Mtambi amesema taratibu zinataka kuwepo kamati saba ikiwemo ya usalama na miundombinu na huduma za kijamii na kila moja ina jukumu lake katika kuhakikisha kunakuwepo na ustawi wa jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Mji wa Bunda wakati wa kujadili hoja za ukaguzi zilioibuliwa na CAG kwa halmashauri hiyo kwa mwama wa fedha 2024/25. Picha na Beldina Nyakeke
"Mfano kuna kamati inayojihusisha na msuala ya afya, kamati hii ikifanya vizuri na sisi tukifanya vizuri kwenye kampeni ya kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi , tutakuwa na uwezo wa kuwabaini wajawazito wote na kuwahamasisha kuhudhuria kliniki wakati huo, pia kama kuna changamoto katika kiliniki hizo basi watatoa taarifa mapema ili hatua zichukuliwe na huduma ziwe bora zaidi," amesema.
Amesema usimamizi wa mifumo kuanzia ngazi za chini ukifanyika vizuri kero mbalimbali ndani ya jamii zitapungua au kuisha kabisa, kwani zitakuwa zikipatiwa ufumbuzi wa haraka pale zinapotokea.
Kutokana na mkakati wa Serikali wa kuufanya mkoa huo kuwa wa utalii, amesema hataruhusu kuona uchafu, hivyo kila kiongozi ambaye eneo lake litakutwa na uchafu lazima ataitwa.
Mkazi wa mkoa huo, Nyangai Majura amesema kumekuwepo na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara, chanzo kikubwa ni uchafu.
"Mwaka jana kulikuwa na mlipuko wa kipindupindu kule Musoma vijijini na hii inatokana na ukweli kuwa mazingira yalikuwa machafu, niombe operesheni hii isiishie kwenye mifuko na chupa za plastiki,” amesema.
Mkazi mwingine, Msomi Burure amesema inashangaza kuona Mji wa Musoma hivi sasa ukiwa mchafu ilhali miaka ya nyuma ulikuwa miongoni mwa miji vinara kwa usafi nchini.