Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Mtambi atoa agizo la watumishi Tarime Vijijini kuhamia Nyamwaga

Mkuu wa Mkoa wa Mara,Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye kikao cha baraza maalum la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini wakati wa kujadili taarifa ya hesabu za CAG kwa halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • RC Mtambi pia ameagiza watumishi wote wa halmashauri hiyo kuhamia Nyamwaga, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya serikali.

Mara. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini kuhamia na kuishi katika eneo la Nyamwaga lilipo makao makuu ya halmashauri hiyo ifikapo Julai Mosi mwaka huu, akisema hakuna sababu ya kuendelea kuishi mjini Tarime ilhali halmashauri imegawanywa takriban miaka mitano iliyopita.

Mtambi pia ameagiza watumishi wote wa halmashauri hiyo kuhamia katika eneo hilo, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya serikali na kuchochea maendeleo ya eneo la Nyamwaga ambalo amesema limekuwa likikosa uwekezaji wa kutosha kwa muda mrefu.

Ametoa agizo hilo leo Jumatano Juni 24, 2026 wakati wa kikao maalum cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichokaa kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25.

“Mkurugenzi nakutaka uhamie hapa ifikapo Julai mosi wewe na watumishi wako. Haiwezekani unaishi Tarime mjini wakati uwezo wa kujenga nyumba za makazi ya watumishi mnao. Hayo ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali. Hayo mafuta mnayotumia yaelekezeni katika ukaguzi wa miradi ya wananchi vijijini,” amesema Mtambi.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini wakiwa kwenye kikao maalum cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali katika halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25. Picha na Beldina Nyakeke

Ameeleza kushangazwa na hali ya halmashauri hiyo, ambayo kwa mujibu wake inaongoza kwa ukusanyaji wa mapato mkoani Mara, lakini imekosa mikakati ya kuendeleza makao yake makuu na kuyafanya kuwa kivutio cha uwekezaji.

“Pangeni mitaa ya Nyamwaga, uwezo huo mnao. Pigeni barabara za lami ili kuvutia wawekezaji. Nataka kuona mji wa Nyamwaga unakua. Hakuna sababu ya kuendelea kuishi Tarime mjini wakati halmashauri zilishagawanywa,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, RC Mtambi ameagiza uongozi wa halmashauri hiyo kufanya ufuatiliaji wa fedha zaidi ya Sh320.8 milioni za ushuru wa huduma kutoka katika mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambazo hazikuonekana kwenye mapato ya halmashauri.

Amesema fedha hizo zinatokana na asilimia 0.3 ya mauzo ghafi ya dhahabu ambayo kwa mujibu wa sheria inapaswa kulipwa na mgodi huo, akitaka uchunguzi wa nyaraka kufanyika na mapungufu hayo kurekebishwa kwa haraka ili halmashauri ipate stahiki yake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

“Kiasi hiki kimebainika baada ya ukaguzi wa nyaraka na ulinganifu na ofisi ya madini ya mkoa. Hivyo halmashauri ifuatilie ili fedha hizo zilipwe kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Aidha, ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha inawawezesha watu wenye ulemavu kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali, akieleza kuwa baadhi yao wanashindwa kuibua miradi kutokana na ukosefu wa elimu na uelewa.

Amesema wataalamu wa maendeleo ya jamii wanapaswa kuwasaidia wananchi hao kubuni miradi yenye tija, hata kama siyo wao wanaoendesha moja kwa moja, bali wanaweza kuajiri wasimamizi na kunufaika na mikopo hiyo.

Kwa upande wake, Diwani wa Bumera, Deogratius Ndege, ameshauri kuwepo kwa uwazi zaidi katika malipo ya fedha kutoka mgodi wa Barrick North Mara, akitaka halmashauri kushirikishwa rasmi wakati wa makubaliano na malipo.

“Tunaomba tuwe tunashirikishwa wakati wa malipo haya ili tuwe na uelewa wa pamoja wa kiasi kinacholipwa na stahiki ya halmashauri,” amesema.

Naye Diwani wa Kemambo, Rashid Bogomba, amesema mikopo ya asilimia 10 bado haijawanufaisha wananchi wengi kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu fursa hiyo, akitaka wataalamu kwenda kwa wananchi kutoa elimu zaidi badala ya kubaki ofisini.