Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Mtanda aagiza waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi PSSSF, NSSF

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza na wafanyakazi wa mkoa huo kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa wilayani Kwimba.


Muktasari:

  • Hatua hiyo ni baada ya kupewa taarifa kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii inawadai waajiri zaidi ya Sh9 bilioni ya malimbikizo ya michango ya wafanyakazi mkoani Mwanza.

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amemuagiza Katibu Tawala wa mkoa huo, Balandya Elikana kukutana na kukubaliana na waajiri wa mkoa huo namna ya kulipa zaidi ya Sh9 bilioni za malimbikizo ya michango ya wafanyakazi ambayo hawajawasilisha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Akizungumza jana Mei Mosi, 2025 wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kwa Mkoa wa Mwanza imefanyika wilayani Kwimba, Mtanda amesema hiyo ni moja ya changamoto inayowanyima wafanyakazi raha hata wakati wa kuadhimisha siku hiyo.

"Leo endapo mfanyakazi huyu akifariki hatapata mafao yake kwa sabababu alikuwa hawekewi fedha kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii, ndio maana taasisi zimepita hapa zimenuna (wakati wa maandamano) kumbe sababu ni hii...,"amesema.

Ameongeza kuwa, "Namuelekeza Katibu Tawala kuwaita wakurugenzi na waajiri wote kukaa, kujadili na kutengeneza makubaliano ya namna ya kulipa madeni haya, nitakuwa mkali kweli kweli,"

Akizungumzia maslahi ya watumishi, Mtanda amesema Serikali katika kipindi cha mwaka 2023/24 na 2024/25 imelipa zaidi ya Sh6.8 bilioni ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 3,556, huku watumishi wapya 831 wakiajiriwa kuboresha utendaji kazi.

Baadhi ya watumishi wakiandamana siku ya wafanyakazi iliyofanyika wilayani Kwimba.

Ameongeza kuwa, Serikali imelipa madai ya watumishi 4,015 yasiyo ya mshahara yakiwemo ya likizo, matibabu na uhamisho yenye thamani ya zaidi ya Sh3.2 bilioni pamoja na kuwapandisha madaraja watumishi zaidi ya 9,829 wa kada mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2023/24, huku watumishi 601 wakibadilishiwa kada.

"Watumishi wameendelea kupewa fursa za kujiendeleza ambapo hadi kufikia Aprili, 2025 jumla ya watumishi 528 wapo masomoni katika vyuo mbalimbali. Watumishi 1,352 wameajiriwa katika sekta mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mwanza,"amesema Mtanda.

Kuhusu ajira kwa vijana, Mtanda amesema vikundi 37 vya vijana hadi sasa vimewezeshwa miundombinu ili kufuga samaki kwenye vizimba 161 ndani ya Ziwa Victoria.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa amewataka wafanyakazi ambao hawajahakiki taarifa zao kwenye daftari la wapigakura kwende kuhakiki ili wapate fursa ya kupiga kura na kupata viongozi bora.

"Sisi tunachokifahamu kuwa mwaka huu 2025 ndio mwaka wa uchaguzi, hatuna kauli nyingine. Maandalizi yanafanyika na uchaguzi utafanyika kwa mujibu wa katiba ya Tanzania,"amesema

Awali, Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Mkoa wa Mwanza,  Khalfani Nyungwa ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi ya wafanyakazi na kuiomba iendelee kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo ya  kutowasilishwa michango yao na waajiri kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, kusua sua kwa ulipwaji wa sitahiki za watumishi pamoja na michango mbambali.

 "Tucta tunatoa wito kwa waajiri wote kuhakikisha malipo ya watumishi yanafanyika kabla ya likizo...wasihamishe wafanyakazi kama hawajaandaa malipo yao,"amesema.

Amesema kodi kwenye mishahara bado ni changamoto kwakuwa mishahara yao ni midogo, kodi ni kubwa hasa ikizingatiwa hali ya gharama za maisha imekuwa juu huku akiiomba Serikali kutatua changamoto ya kikokotoo.

"Hatuoni sababu za msingi kuingia malumbano na Serikali na waajiri, tunaomba uagize waajiri wote wahakikishe wafanyakazi wanapotimiza majukumu yao wanapewa stahikii zao. Nasi kama chama cha wafanyakazi tutahakikisha tunawafikia wafanyakazi wote kuwapa elimu ya kutambua wajibu wao,"ameeleza.

RC Mtanda ameahidi kufanyia kazi changamoto zilizopo ndani ya uwezo wake na zilizo nje ya mamlaka yake kuziwasilisha kwa mamlaka husika.