Ridhiwani awaonya watendaji na fedha za Tasaf

Muktasari:
- Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete Katika ametaka akaunti za benki, ulipaji dirishani na mitandao ya simu vitumike kuharakisha malipo ya Mfuko wa Kuondoa Umasikini (Tasaf).
Kibaha. Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka watendaji wa Serikali wanaolipa fedha za Mfuko wa Kuondoa Umasikini (TASAF) kuharakisha malipo kwa wanufaika wakitumia njia tatu za malipo.
Amezitaja njia hizo kuwa ni malipo ya dirishani, kupitia akaunti za benki na mitandao ya simu.
Ridhiwani ametoa maelekeza hayo jana Julai 10, 2023 alipokuwa akizungumza na watendaji na wafaidikaji wa TASAF katika Mtaa wa Miwaleni mjini Kibaha Mkoani Pwani.
"Msije mkaleta maneno au janja janja hapa matokeo yake siku tukaingia kwenye shida ya kuwatia dhiki wananchi wetu na kama upo utaratibu wowote ambao unakwama, Serikali yenu sikivu ya Rais Samia Suluhu Hassan inasema leteni malalamiko sisi tupo tuyafanyie kazi," amesema Ridhiwani.
Pia amewataka watedaji Kibaha wasiwasubiri wanufaika wa mradi huo wao ndio waende kwenye ofisi za kata huku wanajulikana na wasitafute kisingizio cha kutowasaidia wa Tanzania maana Rais Samia alishatoa maelekezo wanufaika watambuliwe.
Naibu Waziri huyo amewahakikishia utayari wa Serikali kuendelea kupambana kuhakikisha inamfikia kila Mtanzania mwenye hali ya Umaskini na kuwa itahakikisha inabadili maisha yao
Mapema kabla ya kuwatembelea wanufaika wa TASAF, Ridhiwani alianza kuzungumza na watumishi wa Serikali ngazi ya Mkoa na wa Halmashauri ya Mji Kibaha, ambapo amewaasa kuacha tabia ya kusemana ovyo, kuwekeana fitna na kufanyiana vituko kwani kwa kufanya hivyo ni kuzorotesha utendaji kazi kwenye maeneo yao.
Awali Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amewataka watumishi wa umma mkoani humo kutekeleza mipango ya maendeleo na kuondoa kero za wananchi ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi (CCM).