Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rift Valley inavyosimama kumpeleka Ruto Ikulu

Muktasari:

  • William Ruto ana amani mno anapokuwa Rift Valley. Akiwa eneo hilo, ana wafuasi wanaompenda na kumtukuza bila kuyumba mithili ya waumini na dini.

William Ruto ana amani mno anapokuwa Rift Valley. Akiwa eneo hilo, ana wafuasi wanaompenda na kumtukuza bila kuyumba mithili ya waumini na dini.

Yote yenye kusemwa kuhusu Ruto, ukifika Rift Valley hawaamini. Msimamo wa jumla ni kwamba Naibu Rais huyo alifanya kazi kubwa kumwingiza Uhuru Kenyatta madarakani mwaka 2013, kisha Rais huyo wa nne wa Kenya akamgeuka naibu wake.

Ya miaka tisa iliyopita, wananchi wa Rift Valley wanayakusanya kama hasira dhidi ya Uhuru. Wanachotaka sasa ni kumweka madarakani Ruto ili iwe fundisho kubwa kwa Uhuru.

Baada ya kuona maisha ndani ya Jubilee si mazuri, Ruto alianzisha chama kipya, United Democratic Alliance (UDA). Jubilee ni chama ambacho kiliasisiwa na Uhuru pamoja na Ruto.

UDA imeleta ushirika wa Kenya Kwanza. Na sasa Rift Valley kwa sasa utadhani kitovu cha Kenya Kwanza kimezikwa eneo hilo kwa jinsi watu wake walivyo na mapenzi makubwa na umoja huo wa kisiasa.

Ukifika Rift Valley utakutana na habari za kumtukuza Ruto jinsi alivyo kiongozi mzuri na kwamba alionyesha utulivu pasipo kuendeshwa na presha za kisiasa pale Uhuru alipofanya maridhiano na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga. Maelewano ya Uhuru na Raila, maarufu kama “The Handshake”, wafuasi wa Ruto hutafsiri kama usaliti wa Uhuru kwa Ruto.

Kutoka kwenye uoto na mashamba ya chai ya Milima Nandi Hills mpaka kwenye mandhari ya kuvutia Pokot Magharibi, ukifika Rift Kaskazini, utakutana na watu ambao hawaambiwi kitu kuhusu Ruto. Kwao Ruto tayari ni rais anayengoja kuapishwa.

Kwa wakazi wa Rift Valley, Raila ambaye ndiye mpinzani mkuu wa Ruto, hana ubavu wa kumshinda Naibu Rais huyo. Raila ambaye ni bosi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), anawania urais kupitia ushirika wa Azimio la Umoja One Kenya.

Eneo la Rift Valley lina utajiri mkubwa wa kilimo. Matarajio ya ushindi kwa Ruto ni makubwa kwao. Na kuhakikisha hawatanii, kwa wingi wao wameita mzimu wa Orkoiyot ili usaidie safari ya Ruto kuingia Ikulu dhidi ya Raila.

Orkoiyot ni mzimu unaominika kuwa na nguvu ya ziada hasa kwa makabila mawili makubwa kutoka kwenye jamii ya Wakalenjin. Makabila hayo ni Nandi na Kipsigis. Wanaamini kwamba Orkoiyot akiibariki safari ya Ruto, hakuna wa kuzuia.

Jamii ya Wakalenjin ina jumla ya makabila saba, ukiacha ni Nandi na Kipsigis, mengine ni Tugen, Marakwet, Sengwer, Pokot na Sebei. Yote hayo kwa umoja wao wapo mguu mmoja na Ruto.

Wakalenjin wanaamini Ruto ni mpambanaji, kwa hiyo hawatishiki safari hii kuwa ulingoni dhidi ya Raila ambaye anasaidiwa na Uhuru, Rais wa Jamhuri ya Kenya.

Nguvu za kisiasa za Ruto zilizoanzia Kabarak, Nakuru hadi Kijiji cha Sugoi, Turbo, kisha zikaondoka Rift Valley na kutua Nairobi, kwa Wakalenjin hawaamini kama kuna mwanasiasa mwingine mwenye ushawishi kama yeye.

Rais wa Pili wa Kenya, Daniel Moi, naye alikuwa Mkalenjin. Na kwa Wakalenjin wengi, tangu Moi alipoondoka madarakani, hawajaona unafuu wa maisha. Kutoka kwa Mwai Kibaki (Rais wa Tatu) mpaka Uhuru.

James Kimaiyo ni mzee mwenye umri wa miaka 77. Ni Mkalenjin. Anasema kuwa unafuu wa kimaisha alioushuhudia kipindi cha Moi, haufanani na wakati wowote kwa miongo miwili sasa. Moi aliachia madaraka ya urais mwaka 2002. Miaka 21 iliyopita.

“Tukiwa na Moi, maisha yalikuwa mazuri, na fedha ilikuwa kwenye mzunguko mzuri. Tulikuwa na chakula cha kutosha na watoto shule walipata maziwa. Hayo yote hayapo tena. Kama mtoto wa mkulima, Ruto anawakilisha uwezekano wa kila Mkenya kunyanyuka hadi kuwa rais. Nilimwona alipokuwa anasoma Shule ya Sekondari Wareng,” alisema mzee Kimaiyo.

Aliongeza: “Ruto aliishi na mwanafunzi mwenzake jirani na Kanisa la Jeshi la Uokovu. Mara kwa mara nilikuwa nawapa maziwa, maana walikuwa majirani zangu.”

Mzee Kimaiyo, ameshiriki kila uchaguzi tangu utawala wa kikoloni. Bado ana kumbukumbu nzuri na anapenda kujivunia kama mtu aliyemkuza Ruto kwa sababu alikuwa kijana mpambanaji wa maisha tangu mdogo kwa kuwa alitoka familia maskini.

“Ruto alikuwa anaishi kwenye eneo lenye maji, watu wengi hawakutaka kuishi hapo. Hata hivyo, pamoja na mazingira hayo magumu, Ruto alifanya vizuri shuleni na amefika hapa, anaelekea kuwa Rais wa Kenya. Ruto ni mpambanaji ambaye ataweza kuunyanyua vizuri uchumi wetu,” alisema Kimaiyo.

Msimamo wa Kimaiyo unafanana na walionao Wakalenjin wengi, kwamba kama Ruto atashinda urais, maisha yao yatabadilika na kuwa mazuri mithili ya ilivyokuwa enzi za Moi.

“Uhuru ametuangusha sana. Watu wanakufa lakini serikali haifanyi kitu. Tuna matumaini kuwa Ruto atafanya mambo yawe mazuri,” alisema Tomas Komen, mwenye umri wa miaka 50. Komen ni baba wa watoto watatu, mkazi wa kijiji cha Kesonik, Marakwet Mashariki.

Komen amelalamika kuwa eneo lao wamekuwa wakivamiwa mara kwa mara na majirani na hiyo imesababisha washindwe hata kuandaa mashamba yao kwa ajili ya kilimo.

“Gharama za maisha zipo juu sana. Tunasikitishwa kuona serikali pamoja na nyenzo zake zote za kiusalama, inashindwa kudhibiti majirani wavamizi hata nyakati za kupanda mazao,” alisema Komen.

Jamii ambazo ni jirani na eneo la Rift Valley, zimekuwa zikituhumiwa kuvamia vijiji vya eneo hilo na kupora mifugo. Wananchi wa Rift Valley wana hasira kuona hakuna hatua yoyote ambayo inachukuliwa.