Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ripoti: Tanzania imo, mataifa yenye amani zaidi Afrika

Muktasari:

  • Ripoti mpya ya Taasisi ya Uchumi na Amani (IEP) ya mwaka 2023, imeorodhesha nchi zenye amani zaidi barani Afrika ambapo nchi ya Mauritius ndio iliyoongoza huku Tanzania ikishika nafasi ya 17 na Sudan Kusini ikiburuza mkia.

Dar es Salaam. Tanzania yashika nafasi ya 17 kwa kuwa nchi yenye amani zaidi barani Afrika, huku Mauritius ikiongoza na Sudan Kusini ikiburuza mkia.

 Hii imebainishwa katika ripoti mpya ya Taasisi ya Uchumi na Amani (IEP) ya mwaka 2023, toleo la 17, ikionyesha kuwa Tanzania imeshika nafasi hiyo kwa kupata alama 2.058, huku kidunia ikiwa nafasi ya 91

IEP inatarajia kuuzindua utafiti huo hapo kesho Julai 13, 2023; ambapo, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa (UN), wakati Africa ikiwa na jumla ya nchi 54, dunia ina jumla ya nchi 195.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa nafasi ya Tanzania imetokana na kupata alama 2.058 na kwamba kidunia imekuwa ni ya 91.

Katika ripoti ya taasisi hiyo ya mwaka 2022, Tanzania ilikuwa nafasi ya 16 ikiwa na alama 2.001 na 86 kidunia.

Kulingana na ripoti hiyo, katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, dunia imekuwa na hali duni ya amani, huku alama za wastani za nchi zikizorota kwa asilimia tano. Kati ya nchi 163, 95 zilionyesha kuzorota, wakati 66 zilirekodi maboresho.

Ripoti inazitaja sababu za kuzorota kwa amani ambazo ni migogoro, vifo kutokana na migogoro ya ndani, mahusiano ya nje na nchi jirani, ingawa mgogoro wa Ukraine unatajwa kama ndio msingi wa ongezeko hilo lakini pia migogoro mingine imeonekana hasa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia.

Pia kuzorota kwa usalama na ambapo kuna nchi 59 zilizoshuhudia kuzorota na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa katika mwaka 2022.

Vilevile ripoti inasema pia jeshi limekuwa kielelezo cha kurekodi uboreshaji wa amani kwa mwaka 2023. Ambapo kati ya nchi 163, 109 zimeonyesha kufanikiwa.

Hata hivyo, ingawa wastani wa alama za matumizi ya kijeshi ziliboreshwa, jumla ya matumizi ya kijeshi ya kimataifa yaliongezeka kwa sababu ya kubwa ikitajwa kuwa ni matumizi ya kijeshi kuhusiana na migogoro Ukraine.

Kwa mujibu wa ripoti, wakati Mauritius imeshika nafasi ya kwanza ikipata alama 1.546 huku kidunia ikishika namba 23, nchi ya pili yenye amani barani hapa ni Botswana ambayo imepata alama 1.762 huku kidunia ikishika namba 42.

Nchi ya tatu ni Sierra Leone ikipata alama 1.792 ambapo kidunia ikishika nafasi ya 47 na nchi ya nne ni Ghana yenye alama 1.799 kidunia ikishika nafasi ya 51.

Senegal imeshika nafasi ya tano ikiwa na alama 1.827 huku kidunia ikishika nafasi ya 52. Wakati Madagascar imeshika nafasi ya sita ikiwa na alama 1.846 huku kidunia ikiwa ya 55.

Namibia pia hawakubaki nyuma kwani wamepata alama 1.859 na hivyo kushuka nafasi ya saba Afrika huku ikiwa ya 56 kidunia.

Nafasi ya nane ni imeshikwa na Gambia ikiwa na alama 1.888 huku ya 59 duniani, huku Zambia ikiwa ya tisa Afrika kwa kuwa na alama 1.898 huku kidunia ikiwa 63. Nchi iliyofunga kumi bora za Afrika ni Liberia ikiwa na alama 1.946, huku kidunia ikiwa ya 72.

Sudan Kusini imeburuza mkia kwa Afrika ikishika nafasi ya 44 ikiwa na alama 3.221 ambapo kidunia inashika nafasi ya 160.

Sudan Kusini iliyoburuza mkia inasalia kuwa yenye amani kidogo Afrika na mojawapo ya nchi zenye amani kidogo zaidi duniani.

Nchi hiyo imekumbwa na kuzorota kwa asilimia moja ya alama zake kwa ujumla, kutokana na kuzorota kwa maeneo ya migogoro na vita vinavyoendelea.

Kwa nafasi ya dunia nchi yenye amani zaidi ni Iceland ikifuatiwa na Denmark, Ireland, New Zealand, na ya tano ni Austria.

Nchi za mwisho kidunia ni Jamhuri ya Kidemolkrasia ya Kongo iliyoshika nafasi ya 159, ikifuatiwa na Sudan Kusini nafasi ya 160, Syria nafasi ya 161, Yemen 162, kisha nchi iliyoburuza mkia kidunia ni Afghanistan ikiwa ya 163.