Ripoti yabaini uzembe kifo cha mjamzito Tanga

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Muktasari:

  • Waziri Ummy atoa siku 14 baraza la wauguzi na wakunga kutoa taarifa hatua ilizochukua kwa wahusika.

Handeni. Daktari na muuguzi wamekutwa na makosa ya kiutendaji wakati wa kumpatia huduma Mariam Zahoro (39), mjamzito aliyefariki dunia Novemba 11 mwaka huu katika Kituo cha Afya Kabuku wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, ripoti ya kamati iliyoundwa kuchunguza tukio hilo imeeleza.

Kamati ya kuchunguza kifo cha mjamzito huyo imewataja waliokutwa na hatia hiyo ni Ngaboli Shafuli, aliyekuwa daktari wa zamu usiku anayedaiwa kuchelewa kufika hospitali, licha ya kupigiwa simu huku muuguzi Mussa Yusuph, mtaalamu wa idara ya usingizi ambaye simu yake haikupatikana siku ya tukio alipotafutwa.

Mariam alifariki dunia alfajiri ya Novemba 11 mwaka huu katika kituo hicho cha afya na alikuwa akipatiwa matibabu kwa kile kilichoelezwa kukosa fedha Sh15,000 kwa ajili ya upasuaji na siku tatu baadaye watumishi watatu wa afya walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Handeni, Omary Mkangama.

Akisoma ripoti hiyo mbele ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na wananchi wa Kabuku, Mwenyekiti wa Kamati, Dk Ali Said amesema muuguzi wa zamu alimpigia simu mara kadhaa daktari huyo, ila aliendelea kutoa majibu nakuja na kuchelewa kwa takribani saa mbili.

Kuhusu mtaalamu wa tiba za usingizi, aliendelea kutafutwa lakini simu yake haikupatikana mpaka tukio linatokea, jambo ambalo limeifanya kamati kwa hatua za baadaye kushauri kuongeza mtaalamu mwingine ili wawe wawili.

Amesema makosa mengine yaliyoonekana ni watumishi hao kushindwa kuchukua hatua za ziada katika kuokoa maisha ya mama huyo, kwani gari la wagonjwa lilikuwepo na wangeweza kumpeleka Hospitali ya Mkata, lakini pia walitakiwa kuwasiliana na viongozi wa ngazi za juu kwa msaada zaidi. 

"Muuguzi wa zamu alipiga simu mara kadhaa kumueleza daktari kwamba mgonjwa ana hali mbaya na anatakiwa aje kumfanyia upasuaji, mara ya mwisho alimtumia ujumbe wa simu ambao ulimuelezea kwamba kesho wote tutaonekana wazembe kwa sababu haujafika,” amesema Dk Ali.

Baada ya ripoti hiyo, Waziri Ummy ametoa siku 14 kwa baraza la wauguzi na wakunga nchini kutoa taarifa ni hatua gani wamechukua kwa wahusika wote waliobainika kuwa na makosa ya kiutendaji.

Waziri Ummy amesema zipo hatua  zinaweza kuchukuliwa kwa daktari huyo ambazo ni kupewa onyo, kusimamishiwa leseni yake kwa muda au kufutwa katika orodha ya madaktari, ili asifanye kazi popote nchini na hivyo hivyo kwa muuguzi.

Kuhusu suala la kutozwa Sh150,000 kwa mgonjwa huyo, Waziri Ummy amesema sera ya afya hairuhusu mgonjwa kutozwa fedha, hivyo kudaiwa fedha mgonjwa huyo ni makosa na ipo nje ya utaratibu.

"Sera ya afya ya mwakwa 2007 inasema huduma za matibabu kwa wajawazito, watoto wenye umri wa miaka chini ya mitano na wazee wasio na uwezo itatolewa bila malipo, hatujabadilisha sera ya afya, kwa hiyo hapa leo sihalalishi na sikubali kiwango cha fedha cha Sh150,000 kilichowekwa kwa ajili kupata huduma za upasuaji kwa kinamama,” amesema Ummy.

Mume wa marehemu Mariam, Juma Masambo ameiomba Serikali kuhakikisha waliokutwa na hatia wanachukuliwa hatia, kwani kwa kutotenda kwao kazi vizuri wamemsababisha watoto wake wamekosa mzazi mmoja.

Diwani wa Kabuku, Nurudin Semnangwa ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga wodi katika kituo hicho cha afya, kwani hakuna wodi ya kinamama wala wanaume.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema kwa Halmashauri ya Wilaya Handeni, idadi ya vifo vya wajawazito ilikuwa watano kwa mwaka, ila imepungua mpaka watatu kwa mwaka na kueleza juhudi ya kupunguza vifo hivyo itaendelea kupunguzwa.