RITA yataka taasisi kusajili bodi zao

Muktasari:

  • Katika maadhimisho hayo yanayofanyika jijini Dar es Salaam na Dodoma, RITA imetoa elimu kwa Bodi za Wadhamini ilizozisajili na kufanya marejeo ya Katiba zao pamoja na kutoa maelekezo ya kufanya huduma hiyo kielektroniki.

Dar es Salaam. Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imezitaka taasisi zilizosajiliwa Ofisi ya Msajili na Jumuiya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kusajili Bodi za wadhamini kwa mujibu wa sheria.
Pia RITA imezitaka bodi za wadhamini wa taasisi za kidini ambazo hazikusajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani zinaelekezwa kufanya hivyo.
Hayo yameelezwa leo Januari 24 jjijini hapa na Wakili wa Serikali Peter Mbogoro alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa katika maadhimisha Wiki ya Sheria nchini.
Akifafanua zaidi, Wakili Mbogoro amesema kuwa bodi za wadhamini zilizosajiliwa na RITA zinatakiwa kufanya marejeo ya katiba zao kwa kufanya marekebisho ili kuboresha maeneo kama kuweka ibara inayoainisha chombo cha juu cha taasisi husika (Supreme Authority) kwa taasisi za kidini.
“Pia wanatakiwa kuweka ibara inayoelezea namna ya utatuzi wa migogoro inapotokea ndani ya taasisi, kuweka ibara inayoonesha muda wa ukomo wa wadhamini kukaa madarakani, kuweka ibara inayoonesha sababu za mdhamini au wadhamini kuondoka au kuondolewa madarakani.
“Wanapaswa kuweka ibara inayoonesha idadi ya vikao vya wadhamini kwa mwaka na majukumu yake ikiwa pamoja na wajumbe wanaopaswwa kuhudhuria vikao husika na akidi kwa vikao hivyo,” amesema.
Wakili Mbogoro amesema pia wanatoa elimu kwa umma kuhusu kuandika na kuhifadhi wosia, mirathi na masuala ya ndoa na talaka na kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa.
Kwa upande wake Fatma Jumanne Mkazi wa Mbezi Luis jijini Dar es Salaam ameonesha furaha yake ya dhati baada ya kusajili cheti cha kuzaliwa na kupata elimu kuhusu ya masuala yahusuyo kuandika na kuhifadhi Wosia.
"Elimu ambayo nimeipata kuhusu shughuli zinazofanywa na RITA hasa ya kuandika na kuhifadhi wosia itaniwezesha kuchagua msimamizi sahihi wa mirathi na hii itanisaidia kuepusha migongano katika familia yangu," amesema.