Rotary Club ya Arusha Mount Meru yaanza ujenzi benki ya damu Arusha

Mkurugenzi wa Jembe Trust, Dk Sebastian Ndege
Muktasari:
- Benki hiyo ya damu inayojengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru,itagharimu Sh 680milioni ambapo hadi sasa wameshakusanya Sh 300milioni na itakapokamilika itahudumia wananchi zaidi ya Milioni tatu wa mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani.
Arusha. Katika kuboresha sekta ya afya nchini,Rotary Club ya Arusha Mount Meru kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru,imeanza ujenzi wa benki ya damu mkoani humo ambapo ikikamilika itasogeza karibu huduma hiyo muhimu mkoani humo.
Kwa sasa benki ya damu inayotumika ni ile ya Kanda ambayo iko Moshi mkoani Kilimanjaro umbali wa kilomita 80 kutoka Arusha.
Akizungumza leo Jumapili Julai 6,2025 wakati wa kumsimika Rais mpya wa Club hiyo,Wakili Mosses Mahuna,Mkurugenzi wa Jembe Trust,Dk Sebastian Ndege,amesema wameamua kuungana na Serikali kuboresha sekta ya afya nchini.
Amesema lengo la club hiyo ni kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii na kuhamasisha watanzania kujitolea katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo benki hiyo ambayo ni muhimu katika sekta ya afya.
"Kutokana na umuhimu wa damu,tumeamua kusaidia hospitali ya Mt.Meru yenye uhitaji wa benki ya damu sisi kama wadau wa sekya binafsi tunaona tuna wajibu wa kushirikiana na serikali kwani haiwezi kufanya yenyewe kila kitu lazima tushirikiane nao,"amesema
"Leo mbali na kumuapisha Rais mpya tumefanya changizo kwa ajili ya ujenzi wa benki hiyo na tumeweza kukusanya zaidi ya Sh 77milioni.Tunaamini tukiendelea kuhamasisha watanzania wengine tutafikia lengo,"
"Mahitaji ya damu ni kwa mtu yoyote,tujitolee kwa wingi ili isaidie kupunguza vifo vya mama na mtoto,upasuaji na wagonjwa wengine tushirikiane kusaidiana kufanikisha upatikanaji wa damu haraka na tutafungua vilabu maalum vya uchangiaji damu wilayani,"
Awali Mahuna amesema ujenzi wa benki hiyo utagharimu Sh 680milioni ambapo hadi sasa wameshakusanya Sh 300milioni na kuwa wameamua kuungana na kusaidia Serikali kuboresha sekta muhimu ya afya kwani licha ya juhudi za serikali kuboresha sekta hiyo lazima sekta binafsi ichangie pia.

"Kwa kuwa shughuli tunazofanya ni zile zinazogusa jamii tuko na mradi huu mkubwa ambapo tunashirikiana na Wizara ya Afya kupitia hospitali ya Mt.Meru na tumeshapata eneo pale na tumeanza ujenzi mwezi Mei na utakamilika ndani ya kipindi cha miezi 10,"
"Mradi utasaidia watu zaidi ya milioni tatu wa Arusha na maeneo ya jirani na kwa kuwa Arusha hatuna benki ya damu tunategemea benki ya Moshi ambayo ni umbali wa kilomita 80 hivyo tumeona kuna haja ya ujenzi wa benki hii hapa,tunaomba wadau tushirikiane,"ameongeza
Awali Rais anayemaliza muda wake, Olais Alexander,amesema katika uongozi wake mwaka mmoja uliopita wameweza kutekeleza miradi mikibwa miwili ambayo ni ujenzi wa wodi ya watoto njiti katika hospitali ya St.Elizabeth pamoja na kulipa bima kwa watoto waishio katika.mazingira hatarishi wanaoelelewa katika kituo kimoja jijini hapa.