RPC Manyara apatanisha wakulima na wafugaji

Muktasari:
- Usuluhishi na upatanishi imetajwa kuwa moja ya njia zinazoweza kusaidia kumaliza migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo badala ya kutumia nguvu za ziada ikiwemo kupiga mabomu.
Kiteto. Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi amesema migogoro ya ardhi haitamalizika kwa wananchi kupigwa mabomu badala yake kwa njia ya upatanishi.
Hiyo ni baada ya migogoro kuonekana kuwa tishio la maisha ya wakulima na wafugaji.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chekanao Machi 14, 2023, Katabazi amewapatanisha wakulima na wafugaji wa Kijiji cha Chekanao ambao wamekuwa na mgogoro kwa miaka saba sasa.
"Kwa zaidi ya miaka saba, wakulima na wafugaji wa Kijiji cha Chekanao wamekuwa hawana mahusiano mema na wanapigana mara kwa mara,” alisema Katabazi.
Kufuatia suala hilo, viongozi kadhaa wamekuwa wakiyataka makundi hayo kuacha migogoro kupitia mazungumzo lakini bado imekuwa ikiendelea.
"Huwezi kutatua migogoro ya ardhi kwa kupiga watu kwa mabomu, nimekuja hapa nataka tuzungumze...hivi kuna haja gani ya watu kupigana kwani hatuwezi kuzungumza tukayamaliza,” alihoji Katabazi.
Aliwataka wakulima na wafugaji wa eneo hilo kuacha migogoro kwani haina tija.
"Wanaofanya hii biashara ya kugombanisha watu kwa maslahi yao sasa basi wafugaji na wakulima tukae chini kutatua migogoro yetu wenyewe hakuna sababu ya kutumia mabomu tena kwa hili," amesema Katabazi
"Tushirikiane pamoja kuanzia kesho kila kundi liwe na watu kumi tuanze kazi wote twende pamoja kuona ng’ombe na mashamba ya wenye changamoto tutatue," amesema Katabazi
Mwenyekiti wa Kijiji cha Chekanao amesema baadhi ya watu walipoteza maisha kutokana na mapigano ya wakulima na wafugaji.
"Tulipoteza ndugu zetu ndani ya Kijiji hiki kutokana na migogoro ya ardhi, lakini baada ya kuongea na viongozi wa ngazi za juu walitusikia na kujenga kutuo cha Polisi hapa wakatangaza kuwa ni kituo cha kanda"alisema Mwenyekiti Saramba.
Licha ya uwepo wa kituo hicho, waliomba kuwapo kwa usafiri ili usaidie katika utoaji huduma.
"Mfano hapa kwenye kituo chetu cha Polisi ukipata shida inayohitaji Polisi afike eneo la tukio kwa wakati usitegemee, ni mpaka uende kumchukua Polisi kwa usafiri wako binafsi wao hawana usafiri tunaomba Jeshi la Polisi Makao makuu watuaidie usafiri kama sio gari basi hata pikipiki tu kwanza,” amesema Rukaiya Mohamed ambaye ni Mwananchi Chekanao.