Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rushwa ya ngono bado janga kwa wanahabari

Muktasari:

  • Rushwa ya ngono miongoni mwa wanahabari Tanzania, limekuwa ni tatizo kubwa ambalo limewafanya wadau wa jinsia na sheria kuamua kufanya tafiti mbalimbali ili kubaini chanzo na suluhisho la kupambana na rushwa ya ngono.

Rushwa ya ngono miongoni mwa wanahabari Tanzania, limekuwa ni tatizo kubwa ambalo limewafanya wadau wa jinsia na sheria kuamua kufanya tafiti mbalimbali ili kubaini chanzo na suluhisho la kupambana na rushwa ya ngono.

Mwaka 2021, ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Wanahabari Wanawake Afrika (WIN) ilibaini kuwa, unyanyapaa, kuhukumiwa kabla ya kujitetea, hofu na aibu ndicho chanzo cha wanahabari wengi kuogopa kuripoti matukio ya unyanyasaji wa kijinsia wanayofanyiwa.

Si WIN pekee waliofanya utafiti huu, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) nao walifanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 52 ya wanahabari wanaogopa kutoa taarifa za matukio ya unyanyasaji wa kingono kutokana na hofu na unyanyapaa zaidi.

Katika utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mwaka 2018, ulionyesha kuwa rushwa ya ngono kazini na vyuoni bado ni changamoto kubwa, ikiwamo upande wa wanahabari wa kike.

Ripoti hiyo ilibainisha wanaokumbana na changamoto hiyo ni wanawake ambao wanaenda kutafuta kazi, mabinti wanaombwa sana rushwa ya ngono ili waweze kupewa kazi au hata kupandishwa cheo.

Wanahabari kadhaa wamezungumza na kueleza kwa nini wanachagua kukaa kimya kuripoti matukio ya unyanyasaji badala ya kuweka wazi.

Harrieth Makweta, mwanahabari wa gazeti la Mwananchi anasema: “Nionavyo mimi wengi wamekuwa wakihofia kupoteza kazi zao, hasa wale ambao wanakuwa hawapo stable kwenye ufanisi wa kazi, hivyo wanashindwa kujua mbinu ipi sahihi itawafanya waendelee kusalia makazini,” anasema Makweta.

Makweta anaongeza kuwa, changamoto hii anaiona huwakumba zaidi wafanyakazi wapya na wale ambao hufika katika vyumba vya habari kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo au maarufu kama ‘interns’.

Makweta hajatofautiana na Vicky Kimaro wa Gazeti la Habari Leo, yeye anasema, wengi wanahofu ya kuchekwa na wenzao.

“Wengine wana hofu ya kuzodolewa na wenzao, kujengewa chuki na visasi na mabosi. Wengine hofu ya kuondolewa kazini ukizingatia wengi wanafanya kazi kama vibarua,” anasema Kimaro.

Lakini hata wangeripoti, inaelezwa katika ripoti ya WanInfra kuwa, ni asilimia 42 tu ya kesi zinazoripotiwa ndizo hufanyiwa kazi na nyingi kati ya hizo huishia kwa kuwaonya watuhumiwa, mwathirika kupewa pole na kubembelezwa, kesi kuishia njiani na kuwapa mafunzo wanahabari kuhusu unyanyasaji wa kijinsia.

Mwanahabari wa Kituo cha Clouds Media Group, Ntibashima Edward anasema, wanahabari wanawake wanaogopa kutoa taarifa za rushwa ya ngono pindi wanapokumbana nazo kwa sababu ya kuhofia kupoteza ajira.

“Kubwa kabisa ni kuhofia kupoteza kazi kwasababu wengi wanaowaomba rushwa ya ngono ni viongozi kwenye kampuni zao, au ni waandamizi, kwa hiyo anahisi akitoa taarifa na kuliweka wazi hilo na kiongozi huyo likamfikia anahisi anaweza kujitetea na kampuni ikamwamini kiongozi kuliko yeye kama mfanyakazi wa kawaida,” anasema.


Nini kifanyike

Hata hivyo, wadau wa jinsia wametoa ushauri na maoni kipi kifanyike ili kuondoa au kupunguza rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari.

Mdau wa Habari na Mratibu wa taifa wa Taasisi ya Wanawake katika Vyombo vya Habari (WIN), Dk Joyce Bazira, anasema wanahabari wengi huamua kukaa kimya kwa sababu ya hofu kupoteza kazi na kufanyiwa malipizi.

“Lakini wakati mwingine, wanaogopa kutoa taarifa kwa sababu wahusika hawachukuliwi hatua kali, hiyo inawavunja moyo watendaji wanapoachiwa waendelee kupeta, hii inakatisha tamaa,” anasema Dk Bazira.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Mary Kafyome ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya Tamwa, amewataka wanahabari wanawake wajitambue na wasiruhusu vitendo hivyo. Wavikemee kwa nguvu zote na wasiogope.

Mshauri Mwandamizi wa Afya ya Jamii na Jinsia, Dk. Katanta Simwanza, anasema kundi la wanahabari hawana pa kuzungumzia adha za rushwa ya ngono zinazowakabili na hivyo kuna haja ya kuunda madawati ya jinsia katika vyumba vya habari ili kuwapa jukwaa la kuelezea masaibu yao.

Mbali na majukwa hayo kuzungumzia ukatili wa kingono, yatatumika pia kuzungumzia ukatili wa kijinsia ambao wanafunzi na watumishi vyuoni wamekuwa wakikumbana navyo majumbani na nje ya nyumbani, kama vile ukeketaji, kubakwa pamoja na mimba za utotoni.

Dk Bazira anashauri kuwepo kwa sera za jinsi katika vyumba vya habari na zitumike kutoa mwongozo juu ya ukatili wa kijinsia, haki na wajibu kwa waajiri na waajiriwa.

“Lakini kila mfanyakazi afahamu sera ya udhalilishaji wa kijinsia kwa undani ili akipata shida ajue anafanya nini,” anasema Dk Bazira.

Anasema waandishi, hasa wanawake wajengewe uwezo kwenye maeneo yanayowafanya wawe katika hatari zaidi ya kufanyiwa ukatili wa aina hiyo, kwa mfano habari zako hazitoki kwa sababu unaandika vibaya na hivyo unalazimika kutoa ngono, huyo mwandishi asaidiwe kuandika vizuri.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa WIN Afrika, Jane Godia, bado Afrika ina safari ndefu kabla waajiriwa hawajashawishika na kukubali kuwa endapo kuna udhalilishaji wa kijinsia wanatoa taarifa na hatua zinachukuliwa kwa watendaji wa udhalilishaji huo.