Sababu magari kukwama mpakani

Hali ilivyo katika kituo cha pamoja cha forodha baina ya nchi ya Malawi ya Tanzania eneo la Kasumuru baada ya magari ya shehena za mizigo kuiwa kuingia nchini.

Muktasari:

  • Magari hayo yanadaiwa kuzuiwa takribani mwezi mmoja na nusu, jambo lililoelezwa kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wa Watanzania

Mbeya. Sheria mpya zilizopitishwa na nchi jirani ya Malawi zimeelezwa kuwa chanzo cha kukwama kwa magari zaidi ya 60 yaliyobeba shehena za mizigo ya wafanyabishara wa Tanzania kuingizwa nchini kupitia kituo cha pamoja cha forodha eneo la Kasumulu, Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya.

 Magari hayo yanadaiwa kuzuiwa takribani mwezi mmoja na nusu, jambo lililoelezwa kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara Watanzania ambao walikuwa wakiingiza nchini bidhaa hizo, yakiwamo mazao ya nafaka.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase alisema sheria za nchi hiyo ndio kikwazo cha magari yaliyobeba shehena za mizigo kutoruhusiwa kuingia nchini.

“Unajua changamoto iliyopo ni sheria za nchi jirani ya Malawi kutokuwa wazi, sasa tunachokifanya kama uongozi wa wilaya ni kufuatilia hali ilivyo na kutoa taarifa kwa mamlaka husika za Serikali,” alisema.

Manase alisema kutokana na adha hiyo, kuna sababu mamlaka za Serikali ya Tanzania na Malawi kukutana pamoja na kuzungumza ili kumaliza changamoto hiyo na magari yaliyozuiwa kuruhusiwa kuingia nchini.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alisema suala hilo linashughulikiwa haraka ili kuona ni namna gani shehena za mizigo na magari yaliyozuiliwa yanaingia nchini.

"Tunaendelea kulishughulikia kwa kufanya mazungumzo na nchi jirani ya Malawi, pia kuona sheria zao zikoje, lengo ni kuliweka sana na kujenga uhusiano mzuri wa shughuli za kiuchumi,” alisema Homera.

Diwani wa Njisi, mpakani mwa Tanzania na Malawi, Omary Rashid aliomba Serikali kufanya kila linalowezekana kuondoa mkwamo huo kwa kuwa utaleta athari kubwa kiuchumi na kwa wafanyabiashara waliokuwa wakisafirisha bidhaa kuleta nchini.

Alisema hizo ni changamoto za kiuchumi na kwamba ufike wakati kutambua kuna hasara wanazopata wafanyabiashara wa mazao na kusababisha kushindwa kulipa mikopo kwenye taasisi za kifedha.

Awali Juni 5, mwaka huu wafanyabiashara wa eneo la Kasumulu, mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Malawi walipanga magogo barabarani kushinikiza magari zaidi ya 60 yaliyobeba shehena za mizigo yaliyozuiwa nchini humo kuachiwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya magari hayo kuzuiwa zaidi ya mwezi na nusu na kusababisha mazao yanayosafirishwa kuwa katika hatari kubwa ya kuharibika.