Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu tajiri wa tumbaku Shinyanga kujiua

Kahama. Siku mbili baada ya mfanyabiashara maarufu wa tumbaku mkoani Shinyanga, Safari Manjala (54) kudaiwa kujiua kwa kujipiga risasi chini ya kidevu, inadaiwa marehemu alifikia hatua hiyo baada ya kufilisika.

Hata hivyo, Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kennedy Mgani alipoulizwa Septemba 9, 2023 na Mwananchi, alisema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.

Manjala ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Kata ya Ulowa wilayani Kahama, alijiua Septemba 8, 2023 saa mbili asubuhi baada ya kurudi kutokea kwenye shamba lake la miti kijiji cha Ilomelo, Halmashauri ya Ushetu.

Akizungumza kwa njia ya simu jana kaka wa marehemu, Mihayo Manjala alisema marehemu aliyekuwa akihudumiwa na chama cha msingi (Amcos) Iginhyabalimi, aliingiziwa fedha na kampuni ya Mkwawa siku tatu kabla ya kujiua na kuwalipa wakulima wake wote.

Baada ya kukamilisha malipo hayo kwa wakulima, alianza kulalamika kuishiwa fedha.

“Sijajua vyema lakini aliwalipa wakulima wake wote hela ikaisha, sikuongea naye tangu alipotoka kuwalipa wakulima wake. Marafiki zake waliniambia aliwapigia kuwaambia ana shida na hela,” alisema.

Alisema siku ya kuchukua hatua ya kukatisha uhai wake alipiga simu kwa Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani akitafuta namna ya kupata pesa, hata hivyo mbunge huyo alimwomba amsubiri atoke bungeni, lakini baada ya muda alichukua hatua ya kuondoa uhai wake.

"Muda mwingi marehemu alikuwa akilalamikia kukosa pesa, baada ya kulipwa na yeye kulipa madeni, hiyo inaweza kuwa sababu. Asubuhi alimpigia simu mbunge akimuelezea mambo ya hela, lakini hata nusu saa haikupita akajipiga risasi," alisema Mihayo.

Diwani wa Kata ya Ulowa, Pascal Mayengo alisema siku mbili kabla ya Manjala kujiua, alimweleza tayari ameshaanza kuandaa vitalu vya mbegu ya tumbaku.

“Kwenye maongezi yetu tulizungumzia changamoto ya kampuni ambayo tulifanya nayo biashara kuchelewesha malipo yetu, ila yeye alilipwa wiki moja ilizopita, watu wanajiuliza kwa nini amechukua hatua hiyo,

Nafikiri ni msongo wa mawazo, hali yake ya uchumi iliyumba kipato chake kwa mwaka kilikuwa Sh700 milioni hadi Sh800 milioni lakini mwaka huu alipata Sh160 milioni tu,” alisema.

Alisema kuna wakati mradi wa kituo cha mafuta ya mfanyabiashara huyo kiliacha kutoa huduma jambo ambalo lilimuumiza kichwa mfanyabiashara kutokana na mtikisiko huo wa kiuchumi.

Diwani huyo alisema baada ya kupata taarifa hizo, alimpigia Mbunge wa Ushetu kumuarifu tukio hilo, ndipo alipomueleza kuwa mfanyabiashara huyo kabla ya kuchukua maamuzi hayo, alimpigia kumuomba hela naye akamuomba amalizie vikao vya Bunge ndipo wazungumze vyema.

“Manjala aliniambia atakwenda kwenye vitalu vyake vya mbegu na alipokwenda huko aliporudi alipaki gari lake na kujipiga risasi,” alisema.

Nyongeza na Shija Felician