Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu uchaguzi wa TLS kutikisa

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Profesa Edward Hoseah, akiwa ukumbini kabla ya kutangazwa matokeo yaliyompa ushindi wa nafasi ya urais wa TLS juzi.

Muktasari:

  • Tofauti na vyama vingine vya kitaaluma, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) katika miaka ya karibuni kimeonekana kuwa na mguso wa pekee kwa jamii na kutikisa, hasa pale unapofika msimu wa uchaguzi ambao hufanyika kila mwaka.

Dar es Salaam. Tofauti na vyama vingine vya kitaaluma, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) katika miaka ya karibuni kimeonekana kuwa na mguso wa pekee kwa jamii na kutikisa, hasa pale unapofika msimu wa uchaguzi ambao hufanyika kila mwaka.

Hata hivyo, mwaka huu ambao Profesa Edward Hosea amefanikiwa kutetea nafasi yake ya urais, joto la uchaguzi linalezwa kupungua kidogo.

Profesa Hosea, aliyetumia sera ya “Majadiliano ya Kujenga” alishinda kwa kupata kura 621 dhidi ya wagombea wenzake, Harold Sungusia aliyepata kura 380 na Jeremiah Mtobesya, kura 145.

Kwa mujibu wa wachambuzi, pengine Profesa Hosea aliamua kuja na sera hiyo baada ya kuwapo kwa misuguano ya muda mrefu kati ya TLS na Serikali

Imekuwa ni kawaida kwa viongozi wa TLS kuongoza kwa mwaka mmoja pekee, hata hivyo, Profesa Hosea amechaguliwa kwa mwaka wa pili, licha ya kupata upinzani kutoka kwa wenzake wanaotajwa kuwa pia walikuwa na hoja nzuri za kukijenga chama hicho.


Joto la uchaguzi

Uchaguzi wa TLS umekuwa na harakati na ‘amsha amsha’ siyo tu ndani ya chama hicho, bali hata nje kwa sababu una hamasa kubwa kutokana na majukumu ya chama hicho ambayo ni pamoja na kuishauri Serikali na taasisi zake.

TLS ilianzishwa kwa sheria mwaka 1954 kama chama cha kitaaluma cha mawakili nchini na kifungu cha 4 cha sheria hiyo (Sheria ya Chama cha Mawakili wa Tanganyika), inabainisha majukumu makuu matatu ya taasisi hiyo.

Jukumu la kwanza, ni kuwaunganisha, kuwatetea na kusaidia ustawi wa mawakili nchini. Pili, ni kuishauri Serikali na vyombo vyake kama Bunge na Mahakama. Jukumu jingine ni kusimamia maslahi na ustawi wa jamii ya Watanzania.

Kutokana na nguvu hiyo, chama hicho kimekuwa kikipitia nyakati tofauti za viongozi kulingana na wakati husika, lakini katika miaka ya karibuni, TLS ilikuwa mstari wa mbele katika kuikosoa Serikali huku baadhi ya viongozi wake wakiwa mwiba na ambao hawakuwa tayari kwa majadiliano.

Itakumbukwa kwamba mwaka 2017, Tundu Lissu ambaye kwa sasa ni makamu mwenyekiti Chadema, alichaguliwa kuwa Rais wa TLS na katika kipindi chake kulikuwa na msuguano mkali baina ya TLS na Serikali.

Serikali ilikuwa ikikituhumu chama hicho kufanya siasa kwa kukosoa mambo ambayo yalikuwa yakifanywa na Serikali, badala ya kujielekeza kwenye malengo ya kuanzishwa kwake, jambo ambalo lilizidisha migongano baina ya pande hizo mbili.

Machi 2017, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alitishia kukifuta chama hicho kama kingeacha misingi yake na kuingiza siasa wakati alipokutana na uongozi wa TLS jijini Dodoma.

Mwaka uliofuata, Aprili 2018, wanachama wa TLS walimchagua Fatma Karume kuwa rais wao. Fatma ni mwanaharakati na alikuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya awamu ya tano, hivyo alibeba taswira hiyo ndani ya TLS.

Katika kipindi chake cha urais, misuguano kati ya TLS na Serikali pia iliendelea na hasa pale ilipoonekana kana kwamba chama kimebeba sura ya uanaharakati.

Septemba 20, 2019, Fatma alisimamishwa uwakili na Mahakama Kuu kwa madai ya kuishambulia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na alifikishwa mbele kamati ya maadili ya mawakili kujadiliwa. Kamati hiyo ilimfutia uwakili, hata hivyo alirejeshewa tena Juni 21, 2021.


Sera ya Profesa Hosea

Kutokana na hali hiyo ya misuguano, Profesa Hosea aliamua kuja na sera ya majadiliano ya kujenga, kwa maana ya kukaa pamoja na Serikali ambayo ni mdau muhimu ili kutengeneza mazingira ya kufanya kazi kwa ushirikiano.

Wakati wa mdahalo wa wagombea uliofanyika Aprili 27, Profesa Hosea alibainisha kwamba lengo la sera yake ya majadiliano ya kujenga, ni kuiwezesha TLS kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi zake.

“Nimetumia dhana ya ‘constructive engagement’ ili kuhakikisha kwamba Serikali, Bunge na Mahakama tunashirikiana na kuondoa dhana potofu kwamba hatuwezi kushirikiana na Serikali. Na nyie mmeona wenyewe kwa mwaka wangu TLS imetulia na inafanya kazi professionally (kitaalamu).

“Ukitaka kumtoa nyoka pangoni, usimvamie kibutu, nenda naye constructively (kwa kujenga),” alisema Profesa Hosea.

Alibainisha kwamba katika mwaka mmoja wa uongozi wake, ushirikiano huo umeanza kuzaa matunda ambapo Serikali imekubali kutoa fedha kiasi cha Sh1.2 bilioni kwa ajili ya kujenga kituo cha uamuzi (Arbitration Centre).

“Jambo hili si geni kwa wale wanaofikiri hilo ni jambo la kuhongwa na Serikali, si sahihi. Nairobi Arbitration Centre inafadhiliwa na serikali ya Kenya, hivyo hivyo ukienda Rwanda, kitu kama hiki kinafadhiliwa na serikali.

“Kwa hiyo tusipotoshane kwamba eti tumehongwa na Serikali, Hosea hahongwi na kama mnazungumzia dhana ya kuhongwa, mimi ndiyo gwiji wa mambo ya rushwa,” alisema Profesa Hosea.

Juzi, akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Profesa Hosea alibainisha kwamba licha ya uchaguzi kuwa mgumu, alifanikiwa kushinda kwa sababu wanachama wa TLS wameielewa dhana yake ya majadiliano ya kujenga.

“Pale penye mlango umebana, Hosea ametoboa…lakini nisingetoboa kama si kura zenu...kwa sababu mmeona maana ya contrusctive engagement,” alisema huku akishangiliwa na wanachama wa chama hicho.


Wanasheria wazungumza

Wakili wa kujitegemea, Rainery Songea alisema Profesa Hosea amekuja na sera hiyo kutokana na mazingira yaliyokuwepo huko nyuma ya misuguano na Serikali hadi kufikia hatua ya kutishia kufutwa kwa TLS.

“Baada ya kuona hayo, Profesa Hosea akaja na hii sera ya constructive engagement, kujaribu kuzungumza na Serikali, tukae mezani tuangalie tunapishana wapi na kama kuna tofauti tunaziwekaje pembeni ili tuweze kwenda sawa.

“Kwa hiyo kwa namna moja au nyingine, naona hiyo sera yake inasaidia kwa sababu naona sasa hivi kwenye project (miradi) nyingi za Serikali tumeanza kushirikishwa kwa namna moja au nyingine, Rais anapozungumza anatambua kwamba chama kipo, cha Zanzibar pia kinatambulika,” alisema Songea.

Alisisitiza kwamba hoja yake kubwa ilikuwa ni kurudisha uhusiano kati ya TLS na Serikali ambao ulikuwa umepotea kipindi fulani kiasi cha kuwaumiza baadhi ya wanachama. Alisema hoja hiyo imepokelewa vizuri ndiyo maana amechaguliwa tena.

Mwanasheria kutoka Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT), Clay Mwaifwani, alisema ili kuleta mabadiliko, kuna njia mbili tofauti, ama ufanye harakati za kushinikiza au kukaa meza moja.

Alisema hoja ya msingi ni kupatikana kwa mabadiliko ambayo wanachama wanayataka ndani ya TLS na kwamba watu wanatofautiana mitazamo ya namna ya kufikia mabadiliko hayo, kama ni kushinikiza au majadiliano.

“Profesa Hosea atadaiwa ni jinsi gani aliboresha maslahi ya mawakili na masuala mengine muhimu kwa mawakili. Umetumia njia gani, hiyo ni juu yako.

“Wazungu wana msemo kwamba the end justifies the means, unaweza kuwa umetumia njia ambayo watu hawaitaki lakini ukawaletea matokeo ambayo wanayataka, ile njia yako wataifumbia macho,” alisema Mwaifwani.

Hata hivyo, alisema baadhi ya wanachama wanapata ukakasi kuhusu njia hiyo ya majadiliano, kwa sababu historia inaonyesha vyama vya wafanyakazi vina asili moja duniani kote, nayo ni kuendesha mambo yao kwa kushinikiza na vimekuwa vikisuguana na serikali.

“Watu hawaamini kwamba trade unions (vyama vya wafanyakazi) zinaweza kukaa mezani na serikali na zikamaliza mambo kwa njia ya mazungumzo, ndiyo maana hiyo approach (njia) ya Profesa Hosea inatiliwa shaka na baadhi ya mawakili,” alisema Mwaifwani.

Mwanasheria huyo alisema matarajio ya wananchi ni makubwa zaidi kwa TLS kuliko vyama vingine vyote vya kitaaluma, kwa sababu ya namna ambavyo chama hicho kimejiweka katika miaka mitatu iliyopita kwa kusimamia haki na kuzungumza ukweli.

“Miaka mitatu au minne iliyopita TLS ilipokuwa chini ya Tundu Lissu, baadaye Fatma Karume, baadaye Rugemeleza Nshala, ilikuwa ni TLS ambayo imeji-brand (kujipa sura) kusimamia haki, kuzungumza ukweli hata muda ambao watawala hawafurahishwi na huo ukweli.

“Utakumbuka mwaka 2021 mwanzoni wakati wimbi la tatu la korona lilipopiga, unakuta madaktari wanasema wananchi wamtegemee Mungu, kanisa linasema wananchi watumie tangawizi, Serikali inasema hiki, lakini waliokuwa wanaongelea vitu kwa uhalisia wake, walikuwa ni wanasheria,” alisema Mwaifwani.

Kwa upande wake, wakili kiongozi kutoka kampuni ya Haki Kwanza, Alloyce Komba alisema kuwa anamuunga mkono Profesa Hosea, kwa sababu amezungumzia pia suala la uwekezaji ambalo anadhani litaisaidia TLS.

“Mimi nimemuunga mkono Wakili Hosea kwa uongozi mahiri. Yeye ndiye anayejua anatumiaje hiyo dhana yake kuwaunganisha mawakili na kutetea taaluma ya uwakili,” alieleza.