Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu vigogo CCM kufyekwa, watoa kauli

Muktasari:

  • Hoja za ukosefu wa maadili ya chama, kuvunja makundi na kupambana na wanaoitwa ‘wahamiaji haramu’ ni miongoni mwa sababu zilizowaangusha vigogo katika uchaguzi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Dodoma. Hoja za ukosefu wa maadili ya chama, kuvunja makundi na kupambana na wanaoitwa ‘wahamiaji haramu’ ni miongoni mwa sababu zilizowaangusha vigogo katika uchaguzi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mbali na hizo, pia Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara), Abdulrahman Kinana aliwahi kunukuliwa kwenye mkutano wake mkoani Kigoma akisema, “CCM itawakata wagombea wenye udini na ukabila.”

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) ilikutana jijini Dodoma juzi, baada ya kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika Jumamosi, vyote vikiwa chini ya mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkutano wa NEC wa kuchuja wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa mikoa na wanaogombea ujumbe wa NEC ulikuwa ufanyika Oktoba 29 baada ya CC Oktoba 28, lakini iliahirishwa hadi juzi.

Katika kikao hicho, NEC ilichuja majina ya wagombea wa nafasi ya wenyeviti wa mikoa na ujumbe wa NEC kupitia mikoa.

Hata hivyo, orodha ya majina ya wagombea hao waliopitishwa hadi tunakwenda mitamboni hayakuwa yametangazwa.

Majina ya wagombea waliopitishwa na NEC na kutangazwa juzi na Katibu wa Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka ni yale ya jumuiya za chama--UWT, Wazazi na UVCCM.

Kulikuwa na taarifa tofauti, moja ikisema majina ya wagombea wa nafasi ya wenyeviti wa mkoa na wajumbe wa NEC yalitumwa kwenye mikoa husika na nyingine zikisema yalikuwa bado chini ya ofisi ya katibu mkuu yakiendelea kuchambuliwa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Mwananchi, majina yaliyokatwa yakiwemo ya wenyeviti 12 waliokuwa wakitetea nafasi zao ni kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za uvunjifu wa maadili ya chama.

Mbali na hivyo, kipindi cha nyuma NEC iliwahi kuwaonya baadhi ya wenyeviti wa mikoa wakiwatuhumiwa kuwa na mienendo inayokiuka maadili.

Pia, kwenye mikutano kadhaa tangu kuanza kwa uchanguzi ndani ya CCM mapema mwaka huu, viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakionya vitendo vya rushwa na upangaji wa safu za uongozi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2025.

Kauli za viongozi hao wakiwemo, Makamu mwenyekiti Kinana, Katibu Mkuu Daniel Chongolo na Shaka ni kwamba watakaobainika kukiuka maadili kwa kupanga safu au kutoa rushwa wangekatwa kwenye orodha za wagombea.

Hata hivyo, bila kutaja sababu, panga la NEC Jumapili limewapitia wenyeviti 12 waliokuwa wakitetea nafasi zao, wakiwemo waliohama CCM na baadaye kurejea.

Mbali na waliokatwa pia kuna waliobadilishwa nafasi za kugombea, mfano aliyekuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaa, Kate Kamba, licha ya kuomba kutetea nafasi hiyo, NEC imemteua kugombea nafasi ya uenyekiti wa UWT Taifa.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk George Kahangwa alisema katika hali ya kawaida, chama chochote cha siasa kinachofanya mambo yake kwa umakini na mantiki nzuri, kinakuwa na vigezo.

“Kwa hiyo ninafikiri na au tutarajie CCM walikuwa na hivyo vigezo na bila shaka vimetumika na kama walikuwa hawana tutajiuliza na kama hawajavitumia ni sawa na vyama vingine kupanga na kutotekeleza,” alisema.

Dk Kahangwa ambaye pia ni Mhandiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema, “katika awamu za kiuongozi, huwa kuna malengo ya kisiasa ambayo awamu fulani ili yatimie unawahitaji (watu fulani), ni kama katika timu ya mpira, kuna unaowaweka benchi na utawatumia kwa majukumu mengine na hao ambao hawajateuliwa kwa kuendana na malengo ya 2025 wameona hawatoshi.”

Mhadhiri huyo alisema, “kujenga dhana kama uliwahi kwenda chama fulani na ukirudi unaonekana hufai, hii inakiharibia chama na Taifa. Kwa sababu vyama vya siasa, ni kwa ajili ya Taifa letu. Vina kazi mbalimbali ikiwemo kutayarisha viongozi.”


Waliomfuata Lowassa

Katika uteuzi huo wa CCM, makada waliohama chama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kumfuata, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa aliyehamia Chadema na kugombea urais na baadaye kurejea CCM, majina yao yamekatwa.

Baadhi ya waliomfuata Lowassa na baadaye kurejea CCM ni Hamis Mgeja aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.

Alijiengua CCM kwenda Chadema na alikuwa mpiga debe wa Lowassa kwenye kampeni, lakini alirejea CCM na ameomba kugombea nafasi ya mwenyekiti mkoa lakini jina lake limekatwa.

Pia, aliyekuwa mbunge wa Kahama, James Lembeli naye jina lake limekatwa. Lembeli naye aliwahi kuhama CCM na kumfuata Lowassa Chadema.

Mbali na hayo, aliyekuwa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu Oktoba 30, 2017 alitangaza kujiondoa uanachama CCM kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa siasa nchini, kisha akahamia Chadema ambako mwaka 2020 aliomba uteuzi wa kuwania urais bila mafanikio.

Hata hivyo, Aprili 30, 2021, Nyalandu katika mkutano maalumu wa CCM alitangaza kurejea CCM na sasa alikuwa anagombea ujumbe wa NEC kupitia Mkoa wa Singida lakini jina lake limekatwa.

Wagombea wengine waliokatwa ni aliyekuwa mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo aliyegombea uenyekiti wa UWT Mkoa wa Singida.

Pia, huko Mwanza aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa katika mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki, NEC imekata jina kwenye nafasi ya mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza.


Wenyeviti wafyekwa

Pia, NEC imeyafyeka majina ya wenyeviti wa CCM mikoa waliochukua fomu kutetea nafasi zao bila kuelezwa sababu za kukatwa kwao.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, makada ambao majina yao yamekatwa na mikoa yao kwenye mabano ni Dk Abel Nyamahanga (Iringa), Beda Alfred Katani (Katavi), Amandus Dismas Nzamba (Kigoma), Samwel Kiboye Nambatatu (Mara), Dorothy Mwamsiku (Morogoro).

Wengine ni Yussuf Nannila (Mtwara), Dk Anthony Diallo (Mwanza), Ramadhani Maneno (Pwani), Rainer Lukarah (Rukwa), Juma Killimbah (Singida), Ellynico Mkola (Songwe) na Henry Shekifu (Tanga).

Shekifu aliyekuwa akitetea nafasi yake ya mwenyekiti wa Mkoa wa Tanga, alishawahi kuwa mbunge na mkuu wa mkoa katika mikoa ya Mtwara na Manyara.

Kwa upande wa Mkoa wa Kagera, aliyewahi kuwa mbunge na kushika nafasi kadhaa za uwaziri, Nazir Karamagi amepitishwa na NEC kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera akishindana na mwenyekiti anayetetea kiti chake Costansia Buhiye.

Pia, baada ya CCM kurejesha kofia mbili za uongozi, mbunge wa Makambako, Deo Sanga amepitishwa na NEC kugombea wenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe.

Sanga aliwahi kuwa mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, lakini zilipoondolewa kofia mbili za uongozi alibaki na ubunge.


Uchaguzi wa mwaka huu

Katika uchaguzi wa CCM mwaka huu kwa mujibu wa Katibu wa Shaka, zaidi ya wana-CCM milioni 2 walijitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama.

Idadi hii ya wagombea kwa mujibu wa Shaka haijawahi kutokea katika chaguzi zote zilizowahi kufanyika kwenye chama hicho.


Watoa neno

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye maarufu namba 3 alikiri jina lake kukatwa huku akisema kwa sasa hawezi kuongea chochote hadi siku ya uchaguzi wa jumuiya ya vijana wa chama hicho ngazi ya mkoa.

Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, Mgeja alisema atazungumza zaidi leo na alipoelezwa taarifa za jina lake kukatwa alisema, “sina neno, ninaheshimu uamuzi wa vikao vya chama.”

Wakati wawili hao wakishindwa kueleza kwa kina, Dorothy alisema chama chetu kina utaratibu na utaratibu na chama ni vikao, “mimi kama mimi, CCM niliingia kwa kukipenda chama, nikaingia na kikubwa nimeanza tangu nikiwa chipukizi na nimeshika nafasi mbalimbali.

“Ni kweli mimi ni miongoni mwa majina ambayo hayakurudi. Sisi wote ni makada wa CCM na tunatakiwa tuheshimu vikao,”
Dorothy alisema.

Kwa upande Shekifu alisema kilichotokea, “ndiyo demokrasia, kutokurudi jina ni utaratibu tuliojiwekea kuwa watu wawe vetted (wachujwe). Tunataka chama chetu kiwe kimoja kisigawanyike.”

Alisema ndani ya chama hicho na mizani ya demokrasia inasema wengi wape hata kama hukubaliani na suala hilo kwa maslahi mapana ya chama.

Kwa upande wake, Nannila alisema “ni mchakato ambao unapita kwenye vikao halali, inawezekana kwa namna moja ama nyingine, mimi kama mcheza mpira tuna mkataba wa miaka mitano, mwingine anaweza kuchukua nafasi,” alisema.

Nyongeza na Raisa Said (Tanga) na Florence Sanawa (Mtwara)