Sabaya awakana washtakiwa wenzake, alia kizimbani

Wednesday January 19 2022
sabaya pic

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (aliyevaa shati nyeupe) akiwa mahakamani.

By Janeth Mushi

Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amekana kuwafahamu watuhumiwa wenzake watano kati ya sita katika kesi ya uhujumu uchumi huku akidai kuwa alitumiwa watu wa kumuua.

Amedai mahakamani hapo kuwa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili na wenzake sita inatokana na sababu za siasa za Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambapo baadhi ya wafanyabiashara na mtu wao aliyeshindwa ubunge wamekuwa wakimshughulikia.

SOMA: Sabaya aanza kutoa ushahidi akieleza alivyokamatwa

Sabaya alishindwa kuongea na kuanza kutoa machozi pale wakili wake, Moses Mahuna alipomtaka kuelezea ushahidi uliotolewa mahakamani juu ya mgawo wa Sh90 milioni wanazodaiwa kuchukua kutoka kwa mfanyabiashara, Fransis Mrosso.

Leo Januari 19, 2022 mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, akiongozwa kujitetea na Wakili wake Mosses Mahuna, alidai kutowafahamu watuhumiwa hao na kuwa amewaona mahakamani na wengine alikutana nao Gereza Kuu la Arusha na Kisongo.

Akiendelea kujitetea leo Sabaya amedai kumfahamu mshitakiwa wa tano katika kesi hiyo, Sylvester Nyegu ambaye alidai alikuwa akimuona kama watumishi wanaofanya kazi chini ya ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya Hai, akiwa miongoni mwa watumishi hao.

Advertisement

Kuhusu watuhumiwa Enock Mnkeni, Watson Mwahomange na John Aweyo, alidai kutokuwafahamu na kuwa kwa mara ya kwanza alikutana nao mahakamani hapo Juni 4, 2021 walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.

Kuhusu washitakiwa Jackson Macha na Nathan Msuya amedai kuwaona kwa mara ya kwanza Gereza Kuu la Kisongo, Juni 21, 2021 ambapo walipofikishwa gerezani humo walimuulizia.

"Mshitakiwa huyu wa sita, nilimuona 21/6/2021 waliletwa gerezani akiwa na mshitakiwa wa saba na walipofika gerezani niliambiwa wananitafuta wakaniuliza mimi ndiyo Sabaya, wakasema wameunganishwa kwenye kesi yangu hapo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kuwaona,"

Sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo;

Wakili: Lengai hapa mahakamani alikuja shahidi wa jamhuri namba 13, akasema wakati wa upelelezi wake alienda Kilimanjaro na alipofanya mahojiano na baadhi ya watu akiwemo shahidi wa kwanza aliamwambia wewe hukuwa na mahusiano mazuri na mkuu wako wa mkoa wewe hilo unalizungumziaje?

Shahidi: Mheshimiwa Hakimu huyo shahidi namba moja aliyemweleza shahidi namba 13 hayo, hakuna popote shahidi huyo wa kwanza alipodai mimi nilikuwa DC Hai sikuwa na mahusiano mazuri na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Alichokiwa anafanya shahidi wa 13 wa Jamhuri (Ramadhan Juma) aliacha upelelezi akaenda kuokota aina ya siasa zilizokuwa Kilimanjaro akaleta hapa mahakamani, ni shahidi muongo aliyeacha upelelezi akajiingiaza kwenye siasa akaacha taaluma yake.

Wakili: Sasa bwana Lengai hapa mahakamani alikuja shahidi wa 13 wa Jamhuri anasema katika upelelezi wake alibaini kwamba wewe Sabaya na watu aliowaita vijana wako mliunda genge na mlikutana Point Zone kupanga kwenda kwa Mrosso ili kutenda makosa ya kihalifu wewe una utetezi gani juu ya madai haya?

Shahidi: Hilo ni genge la Ramadhani analipwa wafanyabishara, alizunguka na Reginald Temu ama kwa jina lingine Shukuru.

Maumivu ya wafanyabiashara wa Kilimanjaro kwa ajili ya mtu wao kushindwa ubunge wasiniwekee mimi kwa sababu ni chombo cha dola.

Niliweka uhai wangu rehani nikifanya kazi za Serikali mpaka nikatumiwa watu wa kuniua sasa Ramadhani kama chombo cha dola anatakiwa akae upande wa Serikali sio kutengeneza magenge na kutafuta watu waseme tulimpa Sabaya pesa hiyo si kazi ya Serikali

Wakili: Shahidi huyo wa 13 alisema alipata taarifa fiche akasema uligawa fedha kwa vijana wako pale Tulia, tena anadai mlikuwa chumbani

Sabaya akaanza kulia

Wakili: Mheshimiwa naomba shahidi apumzike kwa sababu kuna mambo yanamfanya apate hisia, nitoe swali hilo nitauliza lingine manake linampelekea shahidi kujisikia vibaya

(Shahidi huyo alipopewa maji ya kunywa alidai amefunga na kukaa kwa muda kidogo kisha kuendelea kujitetea)

Wakili: Hapa mahakamani unashtakiwa kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2021 wewe na watu wengine 6 jumla mnakua 7 unamfahamuje mtu anaitwa Enock Mnkeni?

Shahidi: Simfahamu mhehsimiwa Hakimu hadi tarehe 4/6/2021 tulipopandishwa naye mahakamani

Wakili: Na je unamfahamuje Watson Mwahomange?

Shahidi: Sijawahi kumsikia simfahamu nilisikia jina hilo hadi wakati shauri linasomwa mahakamani 4/6/2021

Wakili: Na je unafahamuje mshitakiwa wa nne John Aweyo?

Shahidi: Simfahamu naye nilimuona siku hiyo 4/6/2021 mahakamani

Wakili: Na je unamfahamusje mshitakiwa wa tano Sylvester Nyegu?

Shahidi: Nilikuwa namuona kama watumishi wanaofanya kazi chini ya ofisi ya Mkurugenzi halmashauri ya Hai, alikuwa miongoni mwa hao watumishi

Wakili: Na kuna mtu anaitwa Jcakon Macha je unamfahamuje?

Shahidi: Huyo tarehe 21/6/2021 aliletwa gerezani akiwa na mshitakiwa wa saba na walipofika gerezani niliambiwa natafutwa,wakaniuliza mimi ndiyo Sabaya wakasema wameunganishwa kwenye kesi yangu,waliponitafuta ndiyo niliwaona kwa mara ya kwanza

Wakili: Sasa kuna mshitakiwa wa mwisho Nathan Msuya huyu yeye naye unamfahamu vipi?

Shahidi: Huyo alikuja na mshitakiwa wa sita walikuja gerezani

Wakili: Kulingana na hati ya mashitaka unakabiliwa na makosa matano,kuendesha genge la kihalifu,rushwa,matumizi mabaya ya ofisi  na madaraka na utakatishaji fedha haramu, wewe kwa ujumla una nini la kusema juu ya mashitaka hayo?

Shahidi: Hayo mashtaka yote siyo ya kweli ni mashtaka ya uongo yametengenezwa  kwa misingi ya kisiasa, yametengenezwa ili kunivuniia heshima na imani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yametengenezwa na wapambe wa mtu aliyedhani mimi ndiyo nimemnyima madaraka ya ubunge Hai na Takukuru hawapaswi kujiingiza kwenye siasa badala ya kuchukua na kupata uhalisia.

Wakili: Ni wakati gani wewe uliwahi kuwa mkuu wa Kikosi kazi (task force)?

Shahidi: Sijawahi kuwa mkuu wa task force yoyote na sijawahi kujitambulisha popote kwamba ni mkuu wa task force

Wakili: Shahidi wa 13 amesema huwezi kununua gari la ya milioni 60 na huna mkopo popote, unazungumziaje hili?

Shahidi: Hiyo si mentality ya kiuchunguzi mentality ya kimasikini

Wakili: Kwanini unasema hivyo?

Shahidi: Ni sheria mahakama Kuu imesema mtu akiwa na hela nyingi wasimshitaki mtu akiwa na hela nyingi walipomshitaki mwenzao wa Takukuru Mhasibu.

Hajaleta slip ya mshahahara wangu kwamba napokea kiasi gani kabla ya kusema nina mkopo mimi ndiyo namueleza Ma Dc akifanya kazi miezi 14 ana uwezo wa kuwa na Sh60 milioni na ni aibu miezi 32 Ma Dc wangekuwa hiyo fedha wangejiuzulu wote.

Mheshimiwa Hakimu angenihoji ningemwambia kule Mkinga, Tanga nina ng’ombe 1400 nimepewa na Mzee Sabaya na Mama Sabaya, angenihoji ng’ombe 70 kwa wastani wanaweza kuwa Sh60 milioni.

Sasa hivi watakuwa wameongezeka mheshimiwa na angenihoji angejua kule Malula, King’ori nina heka 54 nimepewa na wazazi wangu na ninalima.

Kama angenihoji angejua huko Liksale tunakodisha mashamba na mke wangu tunalima mahindi na maharage na kabla ya kukopa huko ningemkopa mke wangu ambaye ana biashara za ujasiriamali na ndogo ndogo.

Hakimu Patricia Kisinda anayesikiliza kesi hiyo ameiahirisha hadi Januari 21,2022 ambapo Sabaya ataanza kuhojiwa maswali ya dodoso.

Advertisement